Martha Karua apata pigo mahakamani

Martha Karua apata pigo mahakamani

Kiongozi wa Chama cha Narc-Kenya, Martha Karua amepata pigo baada ya Mahakama Kuu ya Kerugoya kutupilia mbali ombi lake la kupinga ushindi wa Gavana wa Kirinyaga, Ann Waiguru wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Jaji Lucy Gitari ameitupilia mbali kesi hiyo kwa vigezo kwamba haikuwa na msingi na kumwagiza kulipa kima cha shilinhi milioni 5 cha kugharamikia kesi hiyo. Karua amewakilishwa na mawakili Gitobu Imanyara na PN Kihara huku  Waiguru akiwakilishwa na mawakili Kamotho Waiganjo na Paul Nyamondi.

Ni mara ya pili kwa kesi hiyo kutupilia mbali na mahakama. Mara ya kwanza ilitupiliwa mbali ni Jaji Lucy Gitari mnamo Novemba 15 mwaka 2017. Hata hivyo Karua aliwasilisha rufaa katika Mahakama ya Rufaa ambayo iliiagiza Mahakama Kuu kuisikiliza kesi hiyo upya.

Wakitoa uamuzi wakati huo, majaji wa Mahakama ya Rufaa, Mohammed Warsame, Daniel Musinga na William Ouko waliushtumu uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuitupilia mbali kesi hiyo kwa misingi kwamba haikumtendea haki mlalamishi. Mahakama hiyo vilevile ilimwondolea Karua faini ya shilingi milioni 10 aliyotozwa na mahakama.

Waiguru aliwasilisha kesi katika Mahakama ya Juu kupinga kusikilizwa tena kwa kesi dhidi yake lakini jopo linaloongozwa na Jaji Mkuu, David Maraga lilipinga ombi hilo.