array(0) { } Radio Maisha | Miguna asema hajui kile watu wanachozungumzia na kusema hatua ya Gavana Sonko kumteua kuwa naibu wake ina njama fiche

Miguna asema hajui kile watu wanachozungumzia na kusema hatua ya Gavana Sonko kumteua kuwa naibu wake ina njama fiche

Miguna asema hajui kile watu wanachozungumzia na kusema hatua ya Gavana Sonko kumteua kuwa naibu wake ina njama fiche

Hatimaye wakili Miguna Miguna amezungumzia suala la uteuzi wake kuwa Naibu Gavana wa Kaunti ya Nairobi, wadhifa ambao umesalia wazi kwa miezi minne tangu kujiuzulu kwa Polycarp Igathe. Miguna amesema hana ufahamu kuhusu uteuzi huo, akiutaja kuwa wenye nia fiche. Hayo yakijiri, Kiongozi wa Wengi Bungeni, Aden Duale anamtaka Gavana Sonko kuliondoa jina la Miguna. Mbunge huyo wa Garissa mjini amesema Rais Uhuru Kenyatta anastahili kushauriwa kuhusu anayestahili kuwa Naibu wa Gavana Nairobi kwani ndiye Mwenyekiti wa Jubilee. Ikumbukwe Miguna aliwania ugavana akiwa mgombea huru wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8 na baadaye kutangaza kuwa kiongozi wa vuguvugu la National Resistance Movement NRM, ambayo ilikuwa chini ya Muungano wa NASA.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Beatrice Elachi amesema utaratibu mwafaka haukufuatwa wakati wa kuwasilishwa kwa barua ya uteuzi akisema barau hiyo iliwasilishwa kwake na wakili wa Miguna, jambo analosema linakwenda kinyume na sheria. Kadhalika amesema Sonko anafaa kufuata taratibu zilizotumiwa na mwenzake wa Nyeri Mutahi Kahiga kumteua Naibu wake. Aidha amesema atakapopokezwa stakabadhi ya uteuzi ataiwasilisha katika bunge la kaunti inavyohitajika na bunge hilo litatekeleza majukumu yake. Amesema wanasisitiza hatua mwafaka kufuatwa si tu kuwa suala hili linamhusu Miguna lakini kwa sababu sheria imeratibu utaratibu huo. Amemtaja wakili Miguna kuwa mtu ambaye iwapo ataidhinishwa na kushirikiana na Sonko watafanya kazi vyema.

Kauli ya Elachi inajiri huku wawakilishi wa bunge la kaunti hii wametofautiana kuhusu uteuzi huo. Kiongozi wa Wengi katika bunge hilo, Abdi Guyo amesema Jubilee haiwezi kulikubali jina la Miguna kwani si mwanachama wa Jubilee, na lazima aombe upya uraia wa Kenya. Aidha ameongeza Gavana Sonko kabla ya kufanya uteuzi angefanya mashauriano na washikadau wote hasa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Wake, William Ruto. Kiranja wa Wengi, Mwaura Chege na Mwakilishi wa Wadi ya Ngara Chege Mwaura vilevile wamepinga uteuzi huo. Hata hivyo wawakilishi wanaoegemea NASA wamepongeza uamuzi wa Gana Sonko na kusema umefanywa kabla ya makataa ya siku saba waliyompatia kukamilika.

Kiranja wa Wachache Peter Iwatok amesema Sonko angeshtakiwa iwapo hangefuata agizo la kumteua naibu wake. Imwatok amesema gavana huyo hafai kufanya mzaha kwa kumteua mtu ambaye serikali haitamwidhinisha. Ameongeza kuwa bunge la kaunti halitajihusisha na na mchakato ambao utachangia jina la aliyeteuliwa kutopitishwa na serikali ili kuwahudumia wakazi wa Nairobi. Mwakilishi wa Wadi ya Karen, David Mberia aidha amemtaja Miguna anayefaa kujaza nafasi hiyo na kusema NASA haipingi uteuzi wake. Mberia amesisitiza kwamba Gavana amepewa jukumu la kumteua yeyote amtakaye na aliyehitimu kushikilia nafasi hiyo.