Serikali imeanza kutekeleza sera mpya ya kuwapunguza walinzi wa maafisa wakuu serikalini

Serikali imeanza kutekeleza sera mpya ya kuwapunguza walinzi wa maafisa wakuu serikalini

Serikali imeanza kutekeleza sera mpya ya kuwapunguza walinzi wa maafisa wakuu serikalini, ili kuimarisha utendakazi wa idara za usalama. Magavana ndio wa kwanza kuathirika na mpango huo, baada ya Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinett kuagiza walinzi wa ziada wanaowalinda waondolewe na kumwacha kila gavana na walinzi watano pekee.

Kupitia Msemaji wa Polisi, Charles Owino, Boinett amesema hakuna gavana anayelengwa baada ya Mike Sonko wa Nairobi kulalamikia suala la kupunguziwa walinzi. Hatua hiyo inajiri kufuatia tangazo la mwezi uliopita, lililotolewa na Waziri wa Masuala ya Humu Nchini, Fred Matiang'i wa kusawazisha walinzi wa maafisa wakuu ili kuimarisha usalama wa wananchi.

Hayo yakijiri, Kamishna wa eneo la Nairobi, Kangethe Thuku ametangaza kuwa maafisa 2,000 wa polisi wametumwa kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Nairobi, ili kuimarisha usalama wakati wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.