array(0) { } Radio Maisha | UASU na KUSU zasisitiza kuwa mgomo utaendelea hadi mkataba wao utakapojadiliwa na kutiwa saini na fedha kuwekwa kwenye akaunti zao za benki

UASU na KUSU zasisitiza kuwa mgomo utaendelea hadi mkataba wao utakapojadiliwa na kutiwa saini na fedha kuwekwa kwenye akaunti zao za benki

UASU na KUSU zasisitiza kuwa mgomo utaendelea hadi mkataba wao utakapojadiliwa na kutiwa saini na fedha kuwekwa kwenye akaunti zao za benki

Wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma wameghadhabishwa na hatua ya Wizara ya Elimu, Hazina Kuu na Baraza la Ushauri la Vyuo Vikuu vya Umma IPUCCF, kukosa kutimiza ahadi waliyotoa walipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Elimu wiki iliyopita kwamba watawasilisha mkataba bora kwa vyama vyao ili kusitisha mgomo unaoendelea.

Wakizungumza na wanahabari, viongozi wa vyama vya wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu UASU na KUSU, wamesema badala yake siku ya Jumamosi, IPUCCF iliwasilisha stakabadhi waliyodai kwamba ulikuwa mkataba mwingine, stakabadhi ambayo wameitaja kuwa bandia na ambayo haikuafikia viwango vinavyohitajika kwa mujibu wa sheria. Mwenyekiti wa UASU, Muga K'Olale amesikitishwa na hatua ya Waziri wa Elimu na Makatibu wa Elimu ya Juu na wa Hazina Kuu kwa kutoweka mikakati ya kushughulikia malalamiko waliyoibua.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UASU, Constantine Wasonga ameshinikiza kwamba lazima wapewe mkataba ambao utawaridhisha kabla ya kurejea kazini, huku akisema ule uliowasilishwa na IPUCCF ni kejeli kwa mchakato mzima wa mazungumzo kuhusu mishahara yao. Kadhalika amesema IPUCCF ilisema itajadili masuala mawili tu ambayo hayahusiani na masuala waliyowasilisha. Ameongeza kuwa wanasikitishwa na hatua ya zaidi ya wanafunzi laki sita ambao masomo yao yametatizwa, lakini akasema serikali ndiyo inayofaa kulaumiwa kwa masaibu yao.

Wasonga amesema kuna baadhi ya watu wenye njama ya kutatiza shughuli katika vyuo vikuu ili vyuo wanavyomiliki viendelee mbele. Kadhalika amesema watawachukulia hatua manaibu wakuu wa vyuo ambao wametatiza mazungumzo kuhusu mkataba wao.Wakati uo huo, amewashauri wanachama wao kutorejea kazini hadi mkataba wa mwaka 2017/ 2021 utakapojadiliwa, kutiwa saini na pesa kuwekwa kwenye akaunti zao.

Katibu Mkuu wa KUSU Charles Mukhwaya amesema mazungumzo kuhusu mkataba wao yanaweza kuandaliwa na kukamilishwa kwa siku moja lakini hawaelewi sababu za hilo kutofanyika. Wamemshauri Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati na kuwahusisha washikadau wote iwapo itakuwapo haja ya kufanya hivyo ili suala hilo lishughulikiwe mara moja. Mukhwaya amesema manaibu wakuu wa vyuo hawawezi kuutaja mgomo wao kuwa usio halali kwa kuwa hakuna agizo la mahakama lililoutaja kuwa unaoendeshwa kinyume na sheria. Aidha amesema yeyote anayedai kuwa kuna agizo la aina hiyo, hajawakabidhi agizo hilo rasmi.