array(0) { } Radio Maisha | Mahakama ya Rufaa yatupilia mbali kesi ya kupinga uamuzi wa kudumisha ushindi wa Gavana Mike Sonko

Mahakama ya Rufaa yatupilia mbali kesi ya kupinga uamuzi wa kudumisha ushindi wa Gavana Mike Sonko

Mahakama ya Rufaa yatupilia mbali kesi ya kupinga uamuzi wa kudumisha ushindi wa Gavana Mike Sonko

Gavana wa Nairobi Mike Sonko amepata afueni baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali ombi lililotaka kesi ya kupinga ushindi wake isikilizwe upya. Wakitoa uamuzi huo, majaji Roselyn Nambuye, Gatembu Kairu na Kathurima M’Inoti wameafikiana kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Mbogholi Msagha aliitupilia mbali kesi hiyo kwa kuzingatia sheria, kwa kuwa walalamishi; Japheth Muroko na Zachaeus Okoth, hawakuwa tayari kuendelea na kesi hiyo.

Majaji hao wamesema mahakama inayoshughulikia kesi ya uchaguzi ina nguvu, na kuwa jaji yeyote ana uwezo wa kutupilia mbali kesi wakati mazingira yanaruhusu uamuzi huo kuchukuliwa. Hata hivyo wamesema kuwa kosa la kipekee alilolifanya Jaji Mbogholi hakuiondoa kesi hiyo wakati alipoitupilia mbali.

Walalamishi wameagizwa kulipa shilingi milioni tano kugharimia kesi hiyo. Kupitia mawakili Harrison Kinyanjui na Cecil Miller, Gavana Sonko amesema Jaji Mbogholi alikuwa sawa kuitupilia mbali kesi hiyo kwa kuwa wawili hao hawakuwa na nia ya kuendelea nayo. Ameongeza kuwa kesi hiyo iliahirishwa mara mbili kuwapa nafasi Muroko na Okoth, badala yake wakataka kupewa muda zaidi, ishara kuwa hawakuwa tayari.

Punde baada ya uamuzi huo, wakili John Khaminwa anayewawakilisha walalamishi, amesema watawasilisha kesi katika Mahakama ya Juu kwani majaji hao hawakushughulikia suala la kutishiwa kwa wateja wao.