Kamati ya Bunge yawahoji waliohusika na upasuaji wa mgonjwa kimakosa KNH

Kamati ya Bunge yawahoji waliohusika na upasuaji wa mgonjwa kimakosa KNH

Kitendawili kuhusu upasuaji wa mgonjwa asiyestahili katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, KNH kimeanza kuteguliwa baada ya madaktari waliofanya upasuaji huo kuieleza kamati ya Bunge ya Afya wanachokifahamu kuhusu upasuaji huo. Mmoja wa wauguzi amefichua chanzo cha mkanganyiko huo.

Akizungumza alipofika mbele ya kamati hiyo ya Bunge la Kitaifa, muuguzi huyo aliyejitambulisha kwa jina Mary alipewa muda kujieleza kuhusu namna mgonjwa asiyestahili alivyofanyiwa upasuaji wa ubongo. Amesema mgonjwa huyo kwa jina Samuel Kimani alikuwa katika chumba cha wagonjwa 15 na alipofika katika chumba hicho akaliita jina la John Nderitu ambapo mgonjwa, Samuel Wachira ndiye aliitika huku akionekana kuchanganyikiwa.


Madaktari waliotekeleza upasuaji huo aidha wamesema walizingatia utaratibu wa upasuaji na walibaini kuwapo kasoro wakati walipofanya upasuaji na kugundua kuwa mgonjwa hakuwa na mgando wowote wa damu kichwani, jinsi ilivyonakiliwa katika rekodi za matibabu zilizowasilishwa kwao.

Daktari Michael Magoha ambaye ni mmoja wa madaktari wakuu wa upasuaji aliyetakiwa na madaktari wenza kuingilia kati suala hilo amesema walithibitisha mara kadhaa kutoka kwa wauguzi waliomtayarisha mgonjwa huyo kwa upasuaji kubainisha kuwa ndiye aliyestahili kuhudumiwa ambapo walithibitisha kwamba alikuwa ndiye.

Wiki iliyopita Bodi ya Hospitali ya KNH iliwaagiza wafanyakazi waliosimamishwa kazi kutokana na kisa hicho kurejea kazini huku uchunguzi ukiendelea. Waziri wa Afya, Sisily Kariuki aidha aliagiza kukabidhiwa ripoti ya uchunguzi ya Bodi ya Madaktari na Matabibu kuhusu kisa hicho kufikia wiki hii. Suala hilo ililichangia kusimamishwa kazi kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa KNH, Lily Koros na Mkuu wa Huduma za Kliniki. Tayari wagonjwa waliohusishwa na mkanganyiko huo waliruhusiwa kuondoka hospitalini  siku chache zilizopita.