Madaktari wafichua jinsi mgonjwa asiyestahili alifanyiwa upasuaji KNH

Madaktari wafichua jinsi mgonjwa asiyestahili alifanyiwa upasuaji KNH

Madaktari waliomfanyia upasuaji wa ubongo mgonjwa asiyestahili wamefika mbele ya Kamati ya Afya ya Bunge la Kitaifa kueleza kilichojiri. Madaktari hao wamesema walizingatia utaratibu wa upasuaji na walibainisha kunakasoro wakati walipofanya upasuaji na kugundua kuwa mgonjwa hakuwa na mgando wowote wa damu kichwani, jinsi ilivyonakiliwa katika rekodi za matibabu zilizowasilishwa kwao.

Daktari Michael Magoha ambaye ni mmoja wa madaktari wakuu wa upasuaji aliyetakiwa na madaktari wenza kuingilia kati suala hilo amesema walithibitisha mara kadhaa kutoka kwa wauguzi waliomtayarisha mgonjwa huo kwa upasuaji kubainisha ndiye aliyestahili kufanyiwa oparesheni ambapo walithibitisha alikuwa ndiye.

Awali mmoja wa wauguzi aliyehusika katika kumtayarisha mgonjwa huyo amesema aligundua baada ya muda kwamba alikuwa amemwasilisha mgonjwa asiyestahili. Amesema awali aliita jina la mgonjwa aliyefaa kufanyiwa upasuaji na aliyeitika akawa ni mgonjwa tofauti hali anayosema ilichangia mkanganyiko huo. Aidha amesema mgonjwa huyo alikuwa na dalili za kuchanganyikiwa.

Ikumbukwe tayari wagonjwa wote wawili, Samuel Kimani aliyefanyiwa upasuaji bila kustahili na John Nderitu waliondolewa hospitalini siku chache zilizopita.