Mswada wa Kubadili tarehe ya Uchaguzi kuwasilishwa Bungeni

Mswada wa Kubadili tarehe ya Uchaguzi kuwasilishwa Bungeni

Mswada mpya kuhusu kubadilishwa kwa tarehe ya uchaguzi , kutoka Jumanne ya pili ya mwezi Agosti hadi Jumatatu ya wiki ya tatu ya mwezi Disemba, unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni tarehe 14 Machi mwaka huu.

Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa ambaye ndiye mwasisi wa mswada huo anasema tarehe ya Agosti huathiri shughuli muhimu za nchi, ikiwamo elimu. Mbunge huyo kupitia Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2018, amesema hatua ya mataifa ya Afrika Mashariki kusoma bajeti zao wakati mmoja, imekuwa ikitatizwa kufuatia tarehe hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa mswada wa kujaribu kuibadili tarehe ya uchaguzi kuwasilishwa Bungeni. Mara ya kwanza mswada uliyowasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Ugenya David Ochieng ulikosa kupitishwa mwaka 2015, kwani haikupata uungwaji mkono wa asilimia kubwa ya thuluthi mbili ya jinsia.

Baadhi ya mawakili wakuu, akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa IEBC Isaack Hassan awali walisema kubadilishwa kwa tarehe hiyo kunahitaji kura ya maoni kwa kuwa itaongeza muhula ambao Rais aliye mamlakani atahudumu.  

Kinara wa NASA Raila Odinga ni miongoni mwa walioupinga mswada huo, na kusema ulitumika na utawala uliotangulia kuunyanyasa upinzani.