Wakuu wa elimu kufanya ukaguzi wa jinsi somo la Hisabati linavyofunzwa

Wakuu wa elimu kufanya ukaguzi wa jinsi somo la Hisabati linavyofunzwa

Maafisa wakuu wa elimu wanaendesha shughuli ya kukagua jinsi Somo la Hisabati linavyofunzwa katika shule za msingi nchini, hasa darasa la kwanza na la pili. Shughuli hiyo itaendeshwa katika kaunti nane ambazo ni Taita Taveta, Nandi, Kisumu, Homa Bay, Trans Nzoia, Busia, Laikipia na Nairobi. Ukaguzi huo kwa jina Classroom Observation, utawahusisha maafisa wakuu wa elimu ambao wataketi madarasani na kufuatilia jinsi walimu wanavyofunza.

Shughuli hiyo imeorodheshwa chini ya mpango wa Uboreshaji wa Elimu ya Shule za Msingi, Kenya Primary Education Development, iliyofadhiliwa kwa ruzuku ya shilingi bilioni nane kupitia ushirikiano wa mataifa mbalimbali. Aidha mpango huo unatekelezwa kwa usimamizi wa Benki ya Dunia kuhakikisha viwango vya Hisabati vinaboreshwa katika shule za msingi.