MCHAKATO WA KUMBANDUA WAZIRI MATIANG'I OFISINI WAANZISHWA

MCHAKATO WA KUMBANDUA WAZIRI MATIANG'I OFISINI WAANZISHWA

Mawakili wameanzisha mchakato wa kumwondoa ofisini Waziri wa Masuala ya Humu Nchini, Fred Matiang’i, kufuatia hatua ya kufungwa kwa runinga nne nchini mwezi Januari. Katika kesi iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Milimani, Chama cha Wanasheria LSK vilevile kinataka Waziri wa Mawasiliano Joe Mucheru na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Francis Wangusi kutajwa wasiofaa kushikilia ofisi ya umma, kwa kukiuka katiba kuhusu suala la kupata taarifa.

Kupitia wakili Daniel Musyoka, LSK imesema kwamba Matiang’i, Mucheru na Wangusi waliyazima masafa ya runinga hizo ikiwa adhabu kwa kupeperusha hafla ya kuapishwa kwa Kinara wa NASA Raila Odinga kuwa Rais wa Wananchi tarehe 30 mwezi Januari, hivyo wanafaa kuwajibishwa.

Kwa mujibu wa wakili huyo, hakukuwapo na dharura yoyote iliyochangia serikali kuzima runinga za KTN News, Citizen, NTV na Inooro, ikizingatiwa hakuna mapigano yaliyokuwa yakishuhudiwa nchini. Anasema vyombo vya habari vilikuwa vikitekeleza majukumu yao ya kuupa umma taarifa kuhusu yaliyokuwa yakijiri.

LSK imesema uamuzi wa kuwashtaki watatu hao ni kuhakikisha serikali inaiheshimu Katiba na kuzuia suala sawa na hilo kutokea katika siku za usoni.