Wakuu wa UASU wafika bungeni kujieleza kuhusu mgomo wao

Wakuu wa UASU wafika bungeni kujieleza kuhusu mgomo wao

Huku mgomo wa wahadhiri na wafanyakazi wengine wa vyuo vikuu vya umma ukiendelea kwa wiki ya tatu sasa, imebainika kuwa baadhi ya vyuo havijakuwa vikiwasilisha kwa serikali ada mbalimbali ambazo wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo hivyo hutozwa. Hayo yamefichuliwa leo wakati Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa ilipoandaa mkutano na washikadau mbalimbali wa sekta ya elimu kutafuta suluhu ya mgomo huo.

Wakati wa kikao hicho, Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, UASU aidha kimevishtumu vyuo vikuu kwa kutoa mapendekezo yake kuhusu mikataba wa malipo wa mwaka 2017 - 2021. Aidha kimemshtumu Waziri wa Elimu, Amina Mohamed kwa kusalia kimya huku mgomo huo ukiendelea. Baraza la Ushauri la Vyuo Vikuu, IPUCCF kwa upande wake limetoa wito kwa bunge kuishinikiza Wizara ya Elimu na ile ya Hazina Kuu kutoa fedha za kuwalipa wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo wanaogoma.

 

Akizungumza mbele ya Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa siku chache baada ya kufanya kikao na ile ya Seneti ya Elimu, Katibu Mkuu wa UASU. Constantine Wasonga amesema wahadhiri wako tayari kurejea kazini japo amelishtumu Baraza la Ushauri la Vyuo Vikuu IPUCCF kwa kutowaeleza bayana kiwango cha fedha wanachopendekeza katika mkataba wa malipo wa mwaka 2017_2021.


Kwa mara ya kwanza Baraza hilo la Vyuo Vikuu limefichua mbele ya bunge kwamba pendekezo lake kuhusu mkataba huo ni kima cha shilingi bilioni 6.8 kwa kipindi cha mwaka 2017-2018. Francis Aduol ni Mwenyekiti wa Kamati ya Manaibu wakuu wa vyuo vikuu.

Suala jingine lililoibuliwa na wahadhiri ni la manaibu wakuu wa vyuo kutowasilisha ada mbalimbali wanazotozwa na waajiri wao mfano matazo ya Bima ya Afya, NHIF na yale ya uzeeni, hali inayowasababishia wahadhiri mahangaiko makuu wanapotafuta huduma za afya na wanapostaafu. Ni suala ambalo liliwashangaza pakubwa wabunge akiwamo Julius Melly ambaye ni Mbunge wa Tinderet vilevile Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Elimu.


Hata hivyo Aduol amekiri kwamba kuna matatizo ya kuwasilisha matozo hayo na kusema ni jambo linalostahili kishughulikiwa kwa kina. Hata hivyo amesema ada za malipo ya uzeeni za kima cha shilingi bilioni 1.56 za mkataba wa 2010-2013 na shilingi bilioni 2 za mkataba wa 2013-2017 zinastahili kutolewa na serikali kwani tayari malipo ya fedha hizo yaliidhinishwa.

IPUCCF imetoa wito kwa bunge kuishinikiza Wizara ya Elimu na ile ya Fedha kulishughulikia suala la mgomo wa wahadhiri ili warejee kazini haraka iwezekanavyo. Jumla ya wanafunzi laki sita wameathiriwa na mgomo huo ambao unawahusisha wahadhiri takriban elfu 27.