Prof Githu Muigai ajiuzulu
Prof Githu Muigai ajiuzulu
Suleiman Yeri
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof Githu Muigai amejiuzulu. Taarifa ya kujiuzulu kwake imedokezwa na Rais Uhuru Kenyatta kupitia ujumbe wa twitter. Kadhalika Rais Kenyatta ametumia fursa hiyo  kumpongeza Githu Muigai kwa huduma aliyoitoa kwa takriban miaka sita sasa.
Wakati uo huo Rais amemteua Mkuu wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Paul Kihara Kariuki kuchukua nafasi ya Githu.
Githu Muigai atakumbukwa sana kwa kauli zake dhidi ya mikakati ya upinzani kutisha kujiapisha na wakati wa kesi ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta. Kadhalika alichangia pakubwa kuondolewa kwa kesi zilizokuwa zikiwakabili Wakenya sita katika Mahakama ya ICC.
Katika teuzi nyingine Rais amemteua wakili Kennedy Ogeto kuwa wakili wa serikali nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Njee Muturi. Njee Muturi sasa atakuwa Naibu Mkuu wa Wafanyakazi wa Ikulu. Aidha amemteua aliyekuwa mshauri wake wa masuala ya katiba Abidakadir Muhamed kuwa balozi wa Korea Kusini.