Rais atia saini mswada wa ugavi wa mapato

Rais atia saini mswada wa ugavi wa mapato
Na, Sophia Chinyezi
Rais atia saini mswada wa ugavi wa mapato
Hatimaye Rais Uhuru Kenyatta ametia saini kuwa sheria Mswada wa Ugavi wa Mapato, hatua ambayo sasa itaziwezesha serikali za kaunti kuanza kupokea fedha. Ikumbukwe magavana katika baadhi ya kaunti nchini wamekuwa wakilalama kwamba huduma katika kaunti zao zimelemazwa kufuatia ukosefu wa fedha. Kaunti mbalimbali hazikuwa zimepokea fedha miezi kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, jambo lililochangia mishahara ya wafanyakazi kucheleweshwa.
Hazina ya Kitaifa aidha imeagizwa kuanza kutoa fedha kwa kaunti mara moja baada ya mswada huo kuidhinishwa. Akizungumza baada ya hafla hiyo katika Ikulu ya Nairobi, Rais amesema serikali imejitolea kuhakikisha ugatuzi unafanikishwa, na itaendelea kushirikiana na magavana wanapoendeleza majukumu yao.
Miongoni mwa waliokuwamo ni Naibu wa Rais William Ruto, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Linyua, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka, Kiongozi wa Wengi Bungeni, Aden Duale na mwenzake wa Seneti Kipchumba Murkomen.