Muigai apinga kuapishwa kwa Raila

Na, Beatrice Maganga

Muigai apinga kuapishwa kwa Raila

Harakati za Kinara wa NASA, Raila Odinga kujiapisha kuwa Rais zinaendelea kupata pingamizi huku Mwanasheria Mkuu wa serikali, Profesa Githu Muigai akisema hilo ni kosa la uhaini, yaani treason. Muigai amesema katiba i bayana kwamba anayestahili kuapishwa kuwa Rais ni mtu aliyechaguliwa na wananchi kupitia kura na ushindi wake kutangazwa na Tume ya Uchaguzi, IEBC. Kauli hiyo imesisitizwa na Msemaji wa Serikali, Erick Kiraithe.

Muigai aidha amezikosoa harakati za kubuniwa kwa mabunge ya wananchi zinazoendelezwa na NASA kwenye kaunti mbalimbali akisema uongozi kupitia mabunge hayo hautambuliwi kikatiba. Aidha amesema wanaoendelea kujadili hoja za kubuniwa kwa mabunge hayo wanakiuka agizo la Mahakama Kuu ya Kitui ambayo imeagiza kutoendelea kwa mijadala hiyo hadi itakapofanya uamuzi katika kesi iliyowasilishwa kupinga kubuniwa kwa mabunge hayo.
Muigai aidha amesema huenda kaunti zitakazoelekeza fedha za maendeleo katika kubuniwa kwa mabunge hayo zikawajibishwa kwani hatua hiyo ni ubadhirifu wa fedha za umma.

Hayo yakijiri, Raila ameyakosoa mataifa yanayotoa ushauri kwa Kenya kuhusu namna ya kuendeleza masuala taifa hili. Akiwakosoa wanaopinga harakati zake za kuapishwa, Raila amesema anachopigania ni haki za Wakenya huku akisisitiza kwamba hatambui kuapishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ila anautambua tu uchaguzi wa Agosti nane ambapo anaamini kuwa ndiye aliyeshinda.

Ikumbukwe taifa la Marekani limemwomba Raila kutojiapisha siku ya Jamhuri wiki ijayo. Naibu Katibu Mkuu wa Idara ya Masuala ya Afrika, Donald Yamamoto ameonya kuwa mpango huo huenda ukazidisha mgawanyiko nchini. Akizungumza baada ya kufanya mkutano wa faragha na vinara wa NASA, Yamamoto ameahidi kuhakikisha mazungumzo yanaandaliwa baina ya Kenyatta na Raila ili kutatua utata wa kisiasa ulioko nchini.

Aidha kwa mujibu wa waliohudhuria kikao hicho, serikali ya Marekani imewaonya wanaopinga mazungumzo kuandaliwa baina ya serikali na NASA kuwa huenda wakawekewa vikwazo vya kutozuru Marekani. Tayari NASA imewaandikia barua magavana kumi na mmoja kushirikiana katika kutenga eneo ambalo Raila ataapishwa siku ya Jumanne wiki ijayo