Jubilee yaahirisha uteuzi katika kaunti 11

Na Carren Omae
Kinyume na ahadi ya viongozi wake, uteuzi wa Chama cha Jubilee ambao umeanza Ijumaa kwenye kaunti 21 nchini umekumbwa na sarakasi za kila aina. Ilianzia kucheleweshwa kwa vifaa vya uchaguzi, malalamishi ya wapigakura na wawaniaji sawia, vurugu, madai ya udanganyifu na kuharibiwa kwa vifaa vya kura, bila kusahau taarifa ya kujaribu kuficha uhalisia kutoka kwa chama hicho. Aidha uteuzi huo ulicheleweshwa hadi adhuhuri kwenye maeneo takribani yote.
Sasa hatima ya yote imekuwa kusitishwa kwa uteuzi kwenye kaunti 11, ikizingatiwa kuwa kwenye kaunti 25 zilizosalia, shughuli hiyo itafanyika Jumanne wiki ijayo, na Nairobi siku ya Jumatatu.
Kivumbi kilitifuka wakati wa uteuzi wa Jubilee leo hii. Ni hali iliyosababisha kuahirishwa kwa shughuli hiyo katika kaunti 11 ambazo ni: Narok, Kajiado, Kericho, Bomet, Uasin Gishu, Trans Nzoia, Baringo, Nakuru, Elgeyo Marakwet, Embu na Nandi.  Kaunti nyingine ni Kiambu, Laikipia, Meru na Pokot Magharibi.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju hata hivyo licha ya sarakasi na malalamishi kutolewa, uteuzi utaendelea kwenye kaunti za Murang’a, Kirinyaga, Nyeri na Nyandarua. Kaunti nyingine ambazo uteuzi umeendelea ni Meru, Uasin, Tharaka Nithi, Kiambu na Taita Taveta jumla zikiwa kaunti 10.

Aidha Tuju amewahakikishia wafuasi wa Jubilee kwamba uteuzi huo utakamilika ifikiapo Jumatano ijayo, kabla ya makataa ya IEBC ambayo ni Aprili 26. Hata hivyo amesema yu tayari kuwajibikia visa ambayo vimeshuhudiwa huku, akiwaomba msamaha wanajubilee.

Tuju akiwa ameandamana na Mwenyekiti wa Kitaifa wa Bodi ya Uchaguzi Andrew Musangi hata hivyo wametaja chanzo cha uchache wa karatasi za kura kuwa visa vilivyoshuhudiwa . Wamesema hawakutarajiwa idadi kubwa ya watu kujitokeza kushiriki shughuli ya leo.