SECTIONS
Premium

Watu 11 wauliwa Namariat, Turkana

Takriban watu 11 wakiwamo maafisa wa polisi, wameripotiwa kuuliwa usiku wa kuamkia Jumapili na wahalifu wenye silaha kali katika tukio la wizi wa mifugo, huko Namariat, Turkana Mashariki katika kaunti ya Turkana.

Walioliwa ni maafisa wanane wa polisi, chifu wa eneo la Lepeito na wanakijiji wawili wa Namariat.

Msemaji wa polisi Bruno Shioso, amesema maafisa wa polisi waliouliwa walikuwa wakiwafuatilia majangili waliojihami kwa silaha kali, ambao walikuwa wamekivamia kijiji cha Namariat na kuiba idadi kubwa ya mifugo.

Kwa mujibu wa Shioso, oparesheni kali imeanzishwa ili kuimarisha usalama katika eneo hilo.

Hiki ni kisa cha kwanza cha uhalifu mkubwa kutokea katika eneo hilo la Namariat katika kaunti ya Turkana chini ya utawala wa Rais William Ruto.

Akiwa katika kaunti ya Baringo Jumamosi, Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambaye awali aliwahi kuwa mkuu wa wilaya DC, amesema serikali imeweka mikakati ya kuimarisha usalama nchini hasa katika eneo la Bonde la Ufa.