SECTIONS

Aukot adai IEBC haikuzikagua vilivyo stakabadhi za walioidhinishwa kuwania urais

Kiongozi wa Chama cha Third Way Alliance Ekuru Aukot sasa anaitaka mahakama kuishurutisha Tume ya Uchaguzi IEBC kuziwasilisha nakala za vitambulisho za wagombea wanne walioidhinishwa kuwania Urais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Akihojiwa katika Spice FM, Aukot amedai kwamba Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati aliweka sharti hilo kwa baadhi ya wawaniaji huku akikosa kuzikagua stakabadhi zilizowasilishwa na wagombea wengine iliowaidhinisha.

Kwa mujibu wa Aukot mchakato mzima wa uteuzi wa wagombea wa Urais ulioendeshwa na IEBC haukuzingatia sheria kwa kuwa Jaji Mrima aliweka wazi kwamba takwa hilo ni kinyume na sheria.

Ameishtumu IEBC kwa kujaribu kutumia kipengele hicho bila kupitishwa kuwa sehemu ya matakwa katika Sheria za Uchaguzi wa Urais.

Ikumbukwe Aukot alikuwa miongoni mwa wagombea urais ambao hawakuidhinisha na IEBC kwa kukosa kuwasilisha nakala hizo hatua iliyomfanya kuwasilisha kesi mahakamani kupinga takwa hilo akisema linakiuka sheria.