SECTIONS

Waziri Magoha awaonya wazazi wanaowahusisha wanao katika siasa

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amewaonya wazazi dhidi ya kuwaruhusu wanao kujihusisha na siasa za uchaguzi mkuu wa Agosti tisa.

Akizungumza jijini Mombasa kwenye Kongamano la Wamiliki wa Shule za Binafsi, Magoha amesema ni wajibu wa wazazi na walezi kuwalea wanao inavyostahili msimu wa siasa.

Waziri Magoha vilevile amewashauri wanafunzi kukataa kutumika kisiasa na badala yake kutumia muda wao kusoma hasa wakiwa nyumbani kwa likizo fupi.

Kuhusu Mtalaa wa Umilisi, CBC Magoha amesema jumla ya wanafunzi milioni 1.2 watajiunga na Shule ya Upili Daraja ya Chini Junior Secondary School kuanzia Januari 2023 na kwamba utaendelea jinsi ilivyoratibiwa.

Kufikia sasa takriban madarasa 6,500 ya kufanikisha CBC yamejengwa katika Shule za Upili za Umma kote nchini Magoha akiwataka wazazi kuunga mkono mfumo huo.

Amesema miakakati ya kufaninisha wanafunzi kujiunga na Gredi ya 7 itakamilishwa na kuwekwa wazi katika kipindi cha wiki tatu zijazo.

Baada ya kuhudhuria kongamano hilo, Magoha amezuru baadhi ya Shule za Binafsi kutathimini utayarifu wao katika utekelezaji wa CBC kabla kuzindua rasmi Shule ya Binafsi ya Sekondari ya Daraja ya Chini ya Mary Joy iliyo katika eneo la Kisimami.