Mpenzi Sautisol,

Natumai u buheri wa afya. Mie ni mzima, hofu na mashaka ni kwako.

Sababu ya kukuandikia waraka huu ni kukufahamisha namnaninavyoendelea. Baada ya wewe kunishauri nisitoe mimba yako kwani mungu akileta mtoto analeta na sahani yake,nilighairi nia ya kufanya hivyo.

Licha ya hayo,nimekumbwa na matatizo si haba. Kama ujuavyo, kwetu ni pakavu.Tangu uhusiano wetu ulipoanza kule kijijini, ulishuhudia namma wazazi wangu waliuza mifugo na hata mazao ya shambani ili niende shuleni. Nashukuru kwa msaada wako nilipokuwa nakuja chuoni.

Nakumbuka vyema nilipokuja kwako Nairobi na kuishi nawe kwa juma moja kabla ya kwenda chuoni. Sijasahau namma tulivyokoga pamoja, tulivyopika pamoja na hata kwenda ziara ya kununua bidhaa pamoja.

Yetu yalikuwa mapenzi ya kipekee. Mabinti wengi walionea usuhuba wetu gere. Kama vile akina Polycap walivyozoea kunikonyezea jicho ulipoangalia kando. Hata hivyo, penzi letu lilidumu siku nyingi na kuwastaajabisha. Mimi na wewe kuonana kimwili lilikuwa jambo la kawaida. Kila mara uliniahidi kuwa hilo halitabadilisha penzi letu. Lakini dunia ni rangi rangile na kitu kinachodumu duniani ni mabadiliko pekee.Tangu nilipokwambia kuwa tayari ushanipachika mimba, ulibadilika.

Nilikuona ukiwa umepiga picha na vidosho wengine kwenye ziara zako za kimziki. Jambo hili limenipa tumbo joto na kunikeketa maini. Sijapata usingizi kwa siku nyingi. Nashangaa kwa nini haupokei simu yangu.Wasemao husema, juzi tu niliskia fununu kuwa unasema mimba hii sio yako. Unasisitiza kuwa nizae mtoto nikupe utamlea. Najua kuwa mungu akileta mtoto analeta na sahani yake. Je, Mungu haleti baba na mama wa mtoto huyo? Mbona agano la kuwa pamoja lisiwe teja?
Nilisahau haya yote kwani mavi ya kale hayanuki. Nilikuwa nimekata kauli kuwa liwe liwalo sitatoa mimba yako.

Kwa miezi sita nimejizatiti kulea mimba hii bila msaada wowote kutoka kwako. Nimevumilia masimango na dhihaki kutoka kwa wazazi wangu na hata wanakijiji.

Jana yaliyonifika yalinifika. Nilikuwa kwenye sherehe huko chuoni. Sikusimama kwa muda mrefu .Nilipoketi, nilipata maumivu ya mgongo na baadaye nilipata uvimbe miguuni. Nilipoenda hospitalini, daktari alinieleza kuwa nina shinikizo la damu. Nilitibiwa na kurudi chuoni na mwandani wangu. Hata hivyo, ni kwa majonzi mengi ninapokujulisha kuwa mimba ilitunguka. Kwa hivyo hatuna Kenyatta, Mandela, Lupita au Maathai. Uvumi kuwa nilitoa mimba yako ni porojo. Mahasidi wetu wana nia ya kukusumu dhidi yangu. Singeweza kufanya jambo kama hilo kwa mwana wetu.

Yote tisa, kumi ni kwamba bado nakupenda kama uchi wa samaki majini. Sina mengi ni hayo tu. 

Wako wa Ubani, Nerea.