Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto, pamoja na vinara wa CORD, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka, walipotembelea hospitali ya wanajeshi ya Defence Forces Memorial Hospital. (Picha: Kwa hisani)

Kwanza kabisa, makiwa kwa jamaa, ndugu, marafiki na hata wakenya kwa ujumla,wakati wa maombolezi ya wakenya wenzetu waliofariki katika njia ya utumishi wa taifa sehemu ya El-Adde nchini Somalia. Mungu aziweke pema penye wema roho zenu. Zaidi kwa familia zilizoathirika, Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu.

Ama kwa hakika, penye wazee, hapaharibiki jambo. Ningependa sana kupigia mfano tukio la wiki jana siku ya Ijumaa katika hospitali ya wanajeshi ya Memorial jijini Nairobi. Nilivutiwa kuona mjumuiko wa viongozi wetu wa kisiasa kwa pamoja wakiwafariji waathiriwa waliosafirishwa nchini kwa matibabu zaidi.

Ningependa kuizungumzia picha ya Waheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta akiwa na naibu wake William Ruto kisha kando yake, ni uwepo wa uongozi mzima wa Upinzani nchini CORD chini ya Kiongozi Raila Odinga wa ODM, Kalonzo Musyoka wa Wiper na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya. Hii ilikua picha ya mwaka aisee!

Niliwazia mambo mengi tu baada ya kuitazama picha hii. Kwamfano, ingekua vipi endapo viongozi hawa wangekua wakishirikiana kama hivi katika maswala ya ujenzi wa taifa na hasa vita dhidi ya Ufisadi? Jee inaezekana wote hawa kukaa chini na kushauriana kuhusu changamoto zinazolizonga taifa letu leo, kwa manufaa ya mkenya wa kawaida?

Sisi wakenya huja pamoja wakati tumekandamizwa na matatizo ya usalama wa taifa. Mfano ulidhihirika wazi wakati wa shambulizi la kigaidi katika maduka ya Westgate jijini Nairobi. Huu ndio uzalendo halisi unaotazamiwa machoni mwa ulimwengu.

Turudi kwa swala la ushirikiano wa viongozi wetu wa kisiasa. Natazamia wahusika ninaowazungumzia hapa ni watu wenye hekima.

Na bila shaka kuna wakenya wangependa kuona uongozi huo ukishirikiana katika vita dhidi ya ufisadi na hata katika jitihada za kuimarisha uchumi wetu.

Wavyele walinena yaliopita si ndwele, tugange yajayo. Umri wenu unavyo zidi kusonga, nyinyi kama viongozi munafaa kupalilia mbegu za maendeleo ya siku za usoni na kuzika tofauti zetu.

Nazungumza kama kijana anayedhamiria kulijenga taifa kwa mchango mdogo nilionao. Sizungumzi kama raia wa kigeni,ila Mkenya damu niliyepalilia uzalendo tangu enzi za marehemu Babu,kwamba fitina, chuki, uhasama, ukiritimba na vinginevyo,havijengo ila vinabomoa. Tushikaneni jamani,tutafika.

Ali Manzu ni mtangazaji na mwanahabari wa @KTNLeo wasiliana naye kupitia mitandao ya Kijamiiya twita @Ali_Manzu na pia Facebook Ali Manzu. Pia unaweza kumuandikia kupitia barua pepe [email protected]