Lazima Joho, Kingi na Mvurya wafanye pamoja

Gavana Joho (Kulia) na gavana Mvurya (Kushoto).

Lisemwalo lipo na kama halipo, lipo njiani laja.

Harufu ya mapendekezo ya kikatiba chini ya kipepeo cha BBI inavutia kiasi kwamba wakati wowote, ripoti hii itakabidhiwa walezi wake Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga.

Huku Wakenya wa kawaida wakisubiri kwa hamu mwelekeo wa ripoti hii na mapendekezo yake kikatiba, viongozi chungu nzima wanaotoka majimbo yote 14 ambayo yatajwa kuorodheshwa kwenye mpangilio wa marekebisho yajayo wameanza kujisweka ndani ya maandalizi ya jinsi ya kujipanga baada ya 2022.

Katika jimbo la pwani ambalo linazo kaunti sita (Mombasa, Kwale, Kili?, Tana River, Lamu na Taita Taveta), kunao magavana watatu ambao hawana budi ila kusukumwa waende wajumuike na viongozi wengine wa kitaifa kuhakikisha jimbo lao limejiandaa vipi.

Licha ya kuwa na mwakilishi shupavu ndani nya kamati ya BBI, Professa Saeed Mwaguni, ni jukumu la magavana wanaoondoka uongozi wa mashinani Hassan Joho (001), Salim Mvura (002) na Amason Kingi (003) kuona kwamba hata wao wamehusishwa kikamilifu katika ugavi wa jimbo.

Serikali tatu Yaaminika kwamba, ndani ya mapendekezo ya BBI, huenda kukawa na ngazi tatu za serikali. Kwanza serikali ya kitaifa (National Government) inayoongozwa na Rais, naibu wake, Waziri Mkuu na manaibu wake alafu serikali ya ngazi ya pili ya Jimbo (Regional Government) na ile ya kaunti (County Government).

Yadhihirika wazi kuwa haya majimbo 14 (Regional) yamechomozwa kutoka kwa ile katiba ya Bomas (Bomas Draft) ambayo awali yalitupiliwa mbali na hatimaye kutumika yale mapendekezo ya (Kili? Draft).

Mapendekezo ya Bomas yaliazimia majimbo 14 (mikoa) kutoka ile ya minane ya kale nchini. Kulingana na habari za ndani ya BBI ijapo bado hazijaidhinishwa rasmi, yasemekana majimbo 14 yamependekezwa kuigawa nchi kuambatana na mazingira na kaunti zake hususan kufuatia hesabu ya sensa ambayo ilitolewa hivi punde.

Katika kila jimbo kati ya haya, twagusiwa kuwa huenda kukawa na Wakuu wa kusimamia jimbo na naibu wake (Regional Premier and Deputy RP) pamoja na kamanda atakayechaguliwa na wananchi.

Hii ina maana kwamba jimbo litakuwa na kichwa kitakachosimamia kaunti na mashiani. Magavana Hassan Joho, Salim Mvurya na Amason Kingi wanahitajika kuwa na kikao maalum kama vichwa vya jimbo kutafakari mwelekeo wa BBI kabla ya kusubiri kupangwa na Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.

Thamani ya umuhimu wa jimbo itatokana na umoja wa viongozi hawa.

Hassan Joho Akiwa naibu kinara wa chama cha ODM, hatima yake ya ushirikiano wa karibu na ndani na kinara wake Raila Odinga hauko thabiti kama zamani kwa kuwa mabadiliko ya kisiasa yanayokuja kamwe hayawezi kutabirika iwapo Raila ataelekeza sikio lake zaidi kwa Joho kuliko kwa wapenzi wapya wa “Handisheki’.

Twajua hamu yake ni kutengewa nafasi mojawapo katika mpangilio wa BBI lakini akae akijua kwamba Kenya ina wenyewe na la muhimu ni yeye kurudi chini kushauriana na magavana wenzake wanaostaafu kutoka ngazi ya kaunti, Mvurya na Kingi.

Wakiwa hawana mpango wa kufanya “handisheki’ sheki yao kama Watoto wa jimbo, wote wajue huenda wakalamba “njele” baada ya 2022! Joho ashauriane na wenzake wa Kili?  na Kwale, hatimaye wawaite wenzao kutoka kaunti za Tana River, Taita Taveta na Lamu kuona kwamba nyadhifa zote hususani zile za jimbo (Regional) na kitaifa (National) wamejipanga vipi.

Salim Mvurya Gavana wa Kwale Salim Mvurya anafahamika sana kuwa mtu mwenye msimamo mkali haswa katika siasa ya kijimbo.

Yeye ameinamia sana mashinani mwa kaunti yake kuliko kujihusisha kwenye bolingo ya kaunti na ile ya kitaifa licha ya kuwa wasifa wake upo kwake na mpaka nje ya Kwale.

Kwa kifupi, atakiwa wakati huu wa kizunguzungu cha BBI, kupiga moyo wake pasi na kuvaa miwani ya mbao kuwaridhia magavana wenzake Hassan Joho na Amason Kingi kwa azma ya kuandaa jimbo la pwani katika kupata ugavi wakati mabadiliko ya kikatiba yanaposubiriwa na mwananchi wa kawaida.

Mvura ijapo hajawahi kutangaza kwamba anataka kiti kikubwa cha uongozi wa kitaifa kama alivyowahi mwenzake Joho, yungali na nafasi nzuri ya kupata nafasi ikiwa kutakuwa na mpangilio wa ushirikiano baina yao kama magavana.

Yeye na Gavana Amason Kingi wanao uwezo wa kuwa wakuu wa serikali ya jimbo kutokana na wingi wa wapiga kura wa jamii yao.

Amason Kingi kama kiongozi na wakili, wadadisi chungu nzima wanamuona kama mmoja wa viongozi bora ambao wanaweza kushinikizwa na kuwarai wenzake, Joho na Mvurya wamwaachie kubakia serikali ya jimbo iwapo mapendekezo ya BBI yatapitishwa kabla na baada ya 2022.

Ufasaha wake wa kuzungumza lugha za Kiswahili, Kingereza na Kimijikenda na ufahamu wa ushindani wa ndani wa kimawakili walivyo, wengi wanamuona kana kwamba kwenye mfumo mpya wa kiserikali na kikatiba kama huu unaozungumzwa wa BBI, basi anafaa kuwa miongoni mwa wanajimbo wanaostahili kuwaelekeza wananchi wa kawaida.

Ijapo binaadamu wote hawako sawa na wala kukosa kasoro, uanzilishi wa maongozi ya kikatiba upya, unahitaji mtu mwenye kuelewa sheria.

Usawa wa rasilimali Usawa halisi iwapo yasemwayo kweli yapo ndani ya BBI, basi ni kuwaona magavana hawa watatu wameshikana sasa ili ikiwa kunao ugavi wa vyeo mapema kama viongozi wa majimbo mengine wanavyopigania leo, wananchi wa kaunti tatu kubwa za Mombasa, Kili?  na Kwale kuwaona magavana hawa wameshikana na kufanya “hendisheki” kwa niaba ya jimbo zima.