Wajiri yarekodi kisa cha kwanza cha korona

Idadi ya Kaunti ambazo zimeathirika na virusi vya korona zimeendelea kuongezeka nchini baada ya Wajir kuripoti kisa cha kwanza cha virusi hivyo. Mtu mmoja miongoni mwa kumi na wawili waliothibitishwa kuugua leo hii ni wa Kaunti ya Wajir hivyo kufikisha jumla ya kaunti zilizoathirika kuwa kumi na nne.

Katibu Mkuu wa Utawala wa Wizara ya Afya Rashid Aman amesema saba ni wa Kaunti ya Mombasa, watatu ni wa Kaunti ya Nairobi na mwingine ni wa Kitui.

Wakati uo huo, jumla ya watu kumi na watano waliokuwa wakiugua COVID-19 wameruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kuthibitishwa kupona, hivyo kufikisha idadi jumla ya waliopona nchini kuwa mia moja arubaini na nne.  Aman amesema mikakati inayoendelea kuwekwa na serikali kudhibiti maambukizi imesaidia pakubwa na kuwaomba Wakenya kutolegeza kamba.

Hata hivyo, watu wengine wawili wamefariki dunia na kufikisha kumi na saba jumla ya waliofariki nchini kutokana na korona.

Jumla ya watu mia saba sabini na saba wamepimwa kwenye kaunti kumi na nne katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita. Kwa jumla waliopimwa mchini ni watu elfu ishirini mia mbili sitini na nane.

Vile vile , Aman amesema mataifa ya Muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yamekubaliana kuhusu namna ya kuwapima madereva wa matrela wanaosafirisha mizigo katika mataifa haya.

Kuhusu kuwapima watu kwa halaiki, shughuli hiyo itaanza kesho mtaani Kagwagware Nairobi ukiwa ni miongoni mwa iliyoathirika zaidi. Partrick Amoth ni Kaimu Mkurugenzi wa Matibabu katika Wizara ya Afya.