Jina ‘Huduma Namba’ halifai!

Kasoro ya jina ya Huduma Namba ni mpangilio wa maneno unaokiuka sintaskia ya Kiswahili.
Serikali ya Jubilee imejipa sifa mbovu – kutoshauriana na washikadau; huwakurupukia tu kijeshijeshi raia wake kila inapotekeleza jambo. Raia nao kwa kutishika, hutii amri zenyewe kikondoo licha ya kuwa katika giza totoro. Kutoshauriana huku kumewafikisha katika upeo wa udhia wataalamu wa Kiswahili, mimi nikiwamo.

Ni nani aliyebuni jina Huduma Namba? Je, wavuti wa www.bomayangu.go.ke? Maswali haya yananikereketa maini. Kutokana na kisomo changu kidogo cha Kiswahili hadi kiwango cha uzamili, ninaiambia waziwazi serikali kuwa majina haya yana kasoro! Ninafahamu fika kwamba si lazima lugha za matangazo, vilevile kaulimbiu ziwe sahihi kisarufi– almuradi kuna mvuto ‘unaonasa’ makini ya walengwa, pia uchache wa maneno. Hata kuchanganya maneno ya lugha mfano Kiswahili na Kiingereza kunakubalika. Kila mtaalamu wa lugha anaelewa fika ukiushi huu, sikwambii umuhimu wake.

Ili kupata utuvu wa moyo, niliwasiliana na Mshirikishi wa Miradi katika Wizara ya Masuala ya Ndani ya Nchi, Bw. Phillip Lemarasia aliyesema, “Lengo letu lilikuwa kupata jina la kuuvutia umma na tayari jina Huduma Namba limetimiza lengo hilo. Hatuwezi kubadili jina hili kwa sasa ikizingatiwa mchakato uliofuatwa” akasema na kuongeza kuwa, “Tangazo la kuunda nembo yake lilichapishwa mitandaoni na magazetini kisha vijana wakapewa fursa kudhihirisha ubunifu wao. Kamati tatu zilitathmini michango yote na hatimaye mshindi akapatikana…tena ashalipwa shilingi laki tatu. Sidhani kama inawezekana kubadili jina Huduma Namba kwa sasa… Hata hivyo, kabla ya waliosajiliwa kupewa namba rasmi ya huduma, yatakuwapo mashauriano zaidi kuhusu jina lifaalo,” akahitimisha.?

Kasoro ya jina Huduma Namba ni mpangilio wa maneno unaokiuka sintaksia ya Kiswahili. Unapotumia maneno ya lugha moja (huduma na namba), huna budi kuzingatia mpangilio wa maneno katika lugha hiyo kwa kutanguliza neno kuu. Hapa, twazungumzia namba ambayo ni ya kuwahudumia watu. Baada ya neno hilo, yanayofuata yanayotoa tu maelezo zaidi mfano kimilikishi –angu - namba yangu, kiashiria - namba hii, aina kwa njia ya kutambulisha mifano ni namba ya simu, namba ya kitambulisho na namba ya huduma. Katika Kiswahili, hatusemi yangu namba, simu namba, kitambulisho namba, namba huduma wala huduma namba…ni ‘kunajisi’ sarufi. Hebu kupia jicho paspoti yako. Kuna sehemu palipoandikwa namba ya pasi… Katika enzi hii ya kutoshauriana, ingeandikwa pasi namba (kosa).

SEE ALSO :Huduma Namba to gobble up another Sh1 billion

Hivyo basi, majina sahihi ni: Namba ya Huduma au Huduma Number…si Huduma Namba. Aidha, ni aibu kubuni, www.bomayangu.go.ke badala ya www.bomalangu.go.ke kana kwamba Kenya haina wataalamu wa Kiswahili. Boma ni nomino katika ngeli ya LI-YA (umoja - boma langu, wingi - maboma yetu).

Mapuuza haya yamewaudhi sana wapenzi wa Kiswahili. Bw. Henry Indindi (mhadhiri) anasema kwamba, “Taifa linalohiari kutumia ‘bora Kiswahili’ katika shughuli zake rasmi kwa kuwapuuza wasomi na waelekezi kuhusu lugha hiyo, haliwezi kuambiwa chochote kingine ila kusutwa na kuchapwa fimbo za kulitanabahisha. Linasinzia ama kulala sana taifa hili. Msipojihami kwa fimbo za kisawasawa kulitanabahisha, litawaambukiza usingizi,” akahitimisha.

Ahadi ni deni; twasubiri ahadi ya Bw. Lemarasia kwamba kabla ya Wakenya kupewa rasmi namba hiyo ya huduma, mashauriano zaidi ya kupata jina faafu yatafanyika.

For More of This and Other Stories, Grab Your Copy of the Standard Newspaper.

Kauli ya Kifalsafa:

Kushauriana ni jambo jema ikiwa watu watakubaliana nawe, na ni upotezaji wakati iwapo watu hawakubaliani nawe (tafsiri) –Ken Livingstone.

SEE ALSO :Questions for Matiang'i over Huduma Namba

 Mawasiliano [email protected]

Do not miss out on the latest news. Join the Standard Digital Telegram channel HERE.

Get the latest summary of news in your email every morning. Subscribe below

* indicates required
Huduma NambaKiswahiliSintaskia ya kiswahili