Masaibu yanazidi kumkumba Gavana Nanok.

Gavana wa Turkana, Josephat Nanok anazidi kuandamwa na masaibu ya kushtumiwa kutokana na masuala mbalimbali. Mojawapo la masuala hayo ni mabadiliko ya baraza la mawaziri aliyofanya wiki iliyopita.

Mbunge wa Turkana Kusini, James Lomenen amesema kuwa Nanok anapaswa kuwafuta kazi mawaziri hao badala ya kuwahamisha kutoka wizara moja hadi nyingine. Wakazi vilevile wamejawa na ghadhabu kutokana mabadiliko hayo ya baraza la mawaziri.

Gavana Nanok aidha anashtumiwa vikali kwa kushikilia kwamba ni sharti halfa ya kila mwaka ya utamaduni maarufu Tobong Lore iendelea mwezi ujao, na hata kuitengea shilingi milioni 20 za maandalizi, badala yake kuangazia suala la njaa.

Mbali na hayo, wakazi wamejawa na ghadhabu kufuatia hatua ya Nanok sawa na Naibu wa Rais, William Ruto kukwepa kusema ukweli kuhusu makali ya njaa Turkana na vifo vinavyoshuhudiwa.

Ikumbukwe Nanok amekuwa akijikanganya kuhusu suala la njaa. Mara ya kwanza alivilaumu vikali vyombo vya habari hasa runinga akisema vinatia chumvi suala la njaa kwenye kaunti yake. Baadaye alijisifu vyombo hivyo kwa kuangazia suala hilo, hiivyo kuwafanya washikadau mbalimbali kujitokeza kutafuta suluhu.

Tayari magavana wamezindua mpango wa kutoa msaada wa fedha na vyakula mbalimbali ili kuwasaidia waathiriwa wa baa la njaa kwenye kaunti zinazoathiriwa na ukame.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Wycliffe Oparanya anasema kwamba kila kaunti nchini itatoa shilingi milioni moja ili kuzisaidia kaunti 17 ambazo zimeathirika zaidi. Ikumbukwe ni zaidi ya watu milioni 1.2 ambao wanaathiriwa na ukame, ila ni zaidi ya elfu mia nane sitini ambao wameathiriwa zaidi kwenye kaunti 13. Shirika la Msalaba Mwekundu vilevile limezindua mpango wa kukusanya shilingi takribani milioni 800 kuwasaidia waathiriwa wa baa la njaa, japo Wakenya wengi wameonekana kuisusia wakidai kwamba fedha zilizokusanywa katika mpango sawa na huo chini ya kaulimbiu, Kenyans for Kenya mwaka 2011 hazikuwajibikiwa.

We are undertaking a survey to help us improve our content for you. This will only take 1 minute of your time, please give us your feedback by clicking HERE. All responses will be confidential.

TobongloreNanok