Wauguzi waliofeli kusitisha mgomo watafutwa kazi huku wengine wakiajiriwa

Wauguzi wote waliopuuza agizo la Rais Kenyatta lililowataka kusitisha mgomo wao na kurejea kazini tarehe 15 mwezi uliopita watafutwa kazi na wengine kuajiriwa.

Makubaliano haya yameafikiwa wakati wa mkutano wa Rais Kenyatta na baraza la magavana katika ikulu ndogo ya Sagana, kwenye kaunti ya Kirinyaga, ambapo nafasi za wauguzi watakaofutwa zitajazwa  na wengine watakaoajiriwa kwa kandarasi..

Wakati wa maamuzi hayo, Rais amesema Serikali ya Kitaifa itashirikiana na serikali za kaunti katika kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa kwa Wakenya ili kuyakabili magonjwa hatari.

Rais amesema ni lazima wafanyakazi wa umma wawe tayari kushirikiana na serikali katika kutafuta suluhu ya kutatua migogoro ya kikazi bila kuwaathiri wananchi.

SEE ALSO :Pensioners turn to Kenya's DCI in new bid to recover Sh1.2b assets

Wakati uo huo, Naibu wa Rais William Ruto amewasihi magavana kushirikiana na serikali ya kitaifa, katika kuafikia maazimio ya kuimarisha huduma za Afya nchini licha ya kuwapo kwa changamoto kwenye ugatuzi wa sekta ya Afya.

Tarehe 13 mwezi uliopita , Rais Kenyatta alitoa agizo la kuwaagiza wauguzi warejelee majukumu yao ambapo alitaja mgomo wao kuwa haramu. Uamuzi wenyewe ulikosolewa na katibu mkuu wa Muungano wa Vyama vya wafanyakazi COTU Francis Atwoli ambaye alilikosoa baraza la magavana kwa misingi ya kumpotosha rais.

Hata hivyo Chama cha Kitaifa cha Wauguzi, KNUN kupitia katibu wake mkuu Seth Panyako, kilishikilia msimamo wake wa kuendeleza mgomo wenyewe kwa kuyatetea masilahi ya wanachama wake bila woga. Panyako alisisitiza kwamba walikuwa na haki ya kikatiba kugoma.

We are undertaking a survey to help us improve our content for you. This will only take 1 minute of your time, please give us your feedback by clicking HERE. All responses will be confidential.