Bunge kujadili mapendekezo ya Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi

Kwa muda sasa, mjadala umekuwa ukiendelea kuhusu mapendekezo ya Rais Uhuru Kenyatta katika mswada wa kifedha wa mwaka 2018. Lililoibua hisia zaidi ni pendekezo la kupunguza kodi kwa bidhaa za petroli kutoka asilimia kumi na sita hadi nane. Hata hivyo, wabunge wengi wameapa kupinga mapendekezo hayo ya Rais wakisema kuwa licha ya kupunguza, Wakenya wataendelea kuathirika. Si kodi ya thamani za ziada pekee inayowalenga Wakenya katika mswada huo; yapo mapendekezo mengine ambayo yatawazidishia mzigo wa kiuchumi.

Mbali na Kodi ya Thamani ya Ziada ya asilimia nane kwa bidhaa za mafuta, Rais amependekeza kodi ya shilingi kumi na nane kwa kila lita ya mafuta taa. Katika mapendekezo hayo, Rais anasema kuwa anawalenga wafanyabiashara walaghai ambao huyachanganya mafuta taa na petroli kisha kuyauza, kauli ambayo ilisisitizwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich alipofika mbele ya Kamati ya Bajeti jana.

Aidha mapendekezo yanawalenga pia watumiaji wa mitandao na simu ambapo amependekeza ada  ya asilimia kumi na tano. Hatua hii itazidisha ada za mawasiliano ya simu, utumiaji wa mitandao vilevile kuweka na kutoa fedha katika benki iwapo yataidhinishwa na bunge. Kulingana na Rais, kodi ya asilimia ishirini itatozwa wale wanaoshinda katika michezo ya bahati na sibu huku kampuni zenyewe zikitozwa kodi ya asilimia kumi na tano.

Rais pia anawalenga Wakenya walioajiriwa kufanikisha mpango wake wa makazi bora. Kulingana na mapendekezo hayo, Wakenya walioajiriwa watalazimika kulipia asilimia 1.5 ya mishahara yao katika mpango huo huku mwajiri naye akitakiwa kulipia kiwango sawa na hicho kabla ya tarehe tisa kila mwezi.

Katika bajeti ya ziada ya mwaka 2018/ 2019, Rais anapendekeza kupunguzwa kwa jumla ya shilingi bilioni 55 kutoka bajeti. Iwapo Bunge litapitisha mapendekezo ya Rais, basi mgao wa fedha kwa serikali za kaunti utapungua kwa shilingi bilioni tisa.

Kuhusu suala lilo hilo la bajeti ya ziada, Waziri wa Fedha Henry Rotich amependekeza kupunguzwa kwa fedha zinazotengewa Maendeleo ya Maeneo Bunge CDF kwa shilingi bilioni 1.5 na zile zinazotengewa ofisi ya mwakilishi wa kike kwa shilingi bilioni 2.

Kibarua sasa ni kwa wabunge wakati watakapojadili mapendekezo hayo leo hii, ambapo baadhi ya wabunge wa Jubilee na NASA wameahidi kuupitisha , huku baadhi ya wabunge wakiapa kupinga mapendekezo hayo.

Ikumbukwe ili kufanikiwa kuyapinga mapendekezo hayo jumla ya wabunge mia mbili thelathini wanahitajika.