IPOA yasema haina ushahidi wa kutosha dhidi ya polisi

Na, Mate Tongola
IPOA yasema haina ushahidi wa kutosha dhidi ya polisi
Mamlaka ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi, IPOA haijaweza kupokea ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka maafisa wa polisi wanaodaiwa kukiuka haki za waandamanaji waliopinga matokeo ya kura za urais mapema mwezi huu.
Mwenyekiti wa IPOA, Macharia Njeru amekiri kuwa uchunguzi wao umekumbwa na changamoto si haba kukiwamo kukosekana kwa mashahidi na kutokuwapo kwa ripoti zozote kuhusu madai hayo katika mashirika mengine ya kuendesha uchunguzi, ikiwamo ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Keriako Tobiko.
Baada ya visa hivyo kuripotiwa, IPOA ilianza shughuli ya kuchunguza malalamishi yaliyotolewa na wananchi dhidi ya maafisa wa polisi hususan katika mitaa ya Mathare, Huruma, Kibra na Kisumu ambako baadhi ya wenyeji waliandamana kupinga ushindi wa Uhuru Kenyatta dhidi ya Raila Odinga wa NASA.
Ikumbukwe kuwa miongoni mwa waliouliwa wakati wa ghasia hizo ni Samantha Pendo, mtoto wa miezi sita mkazi wa Kisumu na msichana wa umri wa miaka kumi, Stephani Moraa ambaye alipigwa risasi mtaani Mathare, Kaunti ya Nairobi.

Related Topics