Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzindua rasmi mwanzo wa siku mia moja za Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo, wakati uo huo kuwatuma kwenye kaunti mbalimbali madaktari kutoka nchini Cuba

Ikiwa njia mojawapo ya kuboresha afya ya Wakenya na kuiweka Kenya miongoni mwa mataifa yanayotoa huduma bora za kimataifa, Rais Uhuru Kenyatta amezindua Kampeni ya Kitaifa ya Siku 100 ya Utoaji Chanjo, chini ya mpango wa National Rapid Results Initiative, pamoja na madaktari mia moja kutoka Cuba ili waanze kuhudumu kwenye kaunti mbalimbali nchini

Hafla hiyo iliyoandaliwa katika ofisi za Mamlaka ya Usambazaji Vifaa vya Matibabu, KEMSA eneo la Embakasi, Nairobi vilevile ilihudhuriwa na Waziri wa Afya, Sicily Kariuki pamoja na washikadau wegine katika sekta ya afya. Rais amesema serikali imejitolea kufanikisha ahadi yake kwa asilimia mia moja ili kila Mkenya apate huduma bora za matibabu na kwa bei nafuu.

Amesisitiza kwamba mkataba uliowekwa kati ya Kenya na Cuba utaimarisha ushirikiano katika masuala ya afya na kuboresha uwezo wa madaktari wa Kenya katika utendakazi wao.

Wakati uo huo, Rais Kenyatta amesema serikali yake imejitolea kulinda afya ya watoto akiongeza kuwa kutowapa watoto chanjo kunazorotesha afya zao na kuliweka taifa katika hatari ya kukumbwa na mlipuko wa magonjwa hatari. Amezishauri Wizara za Afya na Elimu kushirikiana na kaunti kuweka mikakati ya kuhakikisha watoto wote wanapewa chanjo kabla ya kuanza shule.

Kwa upande wake, Waziri Sicily Kariuki amesema chini ya uongozi wa Rais Kenyatta, Kenya imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya, akitaja mfano wa kupungua kwa idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa kati ya mwaka 2009 na 2015. Kadhalika amesema vifaa vilivyozinduliwa leo vya chanjo ni hatua muhimu katika kuimarisha mifumo ya afya nchini.

Ikumbukwe, hatua ya kuwaleta madaktari kutoka Cuba iliidhinishwa mwezi Machi mwaka huu na Rais Uhuru Kenyatta kufuatia makubaliano baina ya serikali ya Cuba. Aidha, mkataba huo utawawezesha madaktari hamsini wa Kenya kusafiri hadi Cuba kupata mafunzo maalum kuhusu huduma za familia.

Related Topics