DPP apokea faili kumi za uchunguzi wa sakata ya NYS

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji amethibitisha kupokea faili kumi za ripoti ya uchunguzi kuhusu sakata katika taasisi ya Huduma za Vijana kwa Taifa NYS. Noordin amesema amepokea barua kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi DCI George Kinoti kumwarifu kuhusu ripoti hizo za uchunguzi. Aidha amesema kwa sasa kundi maalum katika ofisi yake litazithatimini faili hizo kabla ya kutoa mwelekeo zaidi kuhusu hatua zitakazochukuliwa.

Wakati uo huo, amewahakikishia wakenya kwamba ofisi yake inafanya kila iwezalo kulikabili tatizo hilo, huku akisema jopo kazi maalum lililoteuliwa kuendesha uchunguzi huo, limefanya kazi nzuri kufikia sasa.

Ijumaa wiki iliyopiya Noordin na Kinoti walifanya mkutano wa faragha ambapo walijadili kuhusu taarifa zilizorekodiwa na watu arubaini wanaohusishwa na sakata ya NYS.

Hayo yanajiri huku Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri akitarajiwa kuwasilisha ripoti ya uchunguzi kuhusu sakata ya Ufisadi katika Bodi ya Mazao na Nafaka Nchini NCPB, kwa Tume ya Maadili na Kukabili ufisadi EACC, kesho. Kiunjuri aidha amesema ripoti iliyotayarishwa na Wizara yake, tayari ameiwasilishwa katika Bunge la Kitaifa ambalo litaithatmini kabla ya kuwahoji wanaohusishwa kisha kuwasilisha mapendekezo yake.

Ikumbukwe tayari Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wameagiza uchunguzi wa haraka kufanywa na kuahidi kwamba wanaohusika wataadhibiwa.