Mkenya atambuliwa na jarida la Time la Marekani

Mkenya, Nice Nailantei ametajwa kuwa miongoni mwa watu walio na ushawishi mkubwa mwaka huu, kwa mujibu wa Jarida la Time la Marekani. Nailantei ni mwanaharakati wa vita dhidi ya ukeketaji wa wasichana, vilevile Mkurugenzi Mkuu wa Wakfu wa Kuwalinda Wasichana Dhidi ya Kudhulumiwa, Safe Hands for Girls.

Mkenya huyo ametambuliwa kwa juhudi zake katika shirika la Amref Health Afrika ambalo limewalinda zaidi ya wasichana elfu kumi na tano dhidi ya kukeketwa. Ametajwa kuwa kielelezo hasa katika jamii yake ya Maasi ambapo mila ya ukeketaji ingali inatekelezwa.

Miongoni mwa watu waliotajwa kuwa na ushawishi kubwa na jarida hilo mwaka huu, ni pamoja na Rais wa Marekani Dolad Trump, Mwigizaji Nicole Kidman, Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Arden miongoni mwa wengine.

Orodha hii haizingatii mamlaka wala mali wanaomiliki wanaotajwa, ila ushawishi wao ambao huchangia mabadiliko mbalimbali katika jamii.