Ebola
Taharuki Eldoret
Taharuki imetanda Mjini Eldoret baada ya mwanamume aliyekuwa akisafiri kutoka Kampala Uganda kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Moi akiwa na dalili za ugonjwa wa Ebola. Kwa sasa, hospitali hiyo iko chini ya ulinzi mkali huku wanahabari wakizuiliwa kuingia kwa kuwa hawana vifaa maalumu vya kujikinga dhidi ya maambukizi. Jamaa huyo alikuwa amesafiri kutoka Sudan kusini na kupitia Uganda kabla ya kuwasili Eldoret. Damu yake imepelekwa katika kituo cha utafiti cha KEMRI jijini Nairobi kwa uchunguzi zaidi. Mkuu wa kitengo cha kudhibiti magonjwa katika Wizara ya Afya Willis Akhwale amesema tayari wakuu wa afya katika mikoa ya Nyanza, Bonde la Ufa na Magharibi wametakiwa kuripoti visa vyovyote vinavyohusishwa na ugonjwa huo.
Posted on August 2, 2012 na Mate Tongola
