Ugaidi
Serikali yaimarisha doria kukabili magaidi
Serikali ya Kenya imeongeza idadi ya maafisa wa polisi katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa nchi ili kudhibiti visa vya mashambulizi. Kwenye kikao rasmi cha wanahabari kaimu waziri wa usalama wa taifa Yusuf Hajj amesema baadhi ya mikakati iliyoanzishwa ni wageni wanaofika kwenye miji ya eneo hilo, hotelini na majengo mengine watakaguliwa zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Vilevile serikali imeongeza magari yapolisi kwa mengine 14 kufadhili doria za polisi. Wakati huo huo kufikia sasa, zaidi ya watu 30 wamehojiwa na polisi kuhusiana na mashambulizi ya Jumapili iliyopita Mjini Garissa, ambapo watu 17 wakiwamo maafisa 2 wa polisi waliuawa. Naibu Mkuu wa Polisi Mkoani Kaskazini Mashariki Philip Ndolo ameiambia Radio Maisha kuwa 30 hao wanajumuisha washukiwa 15 wenye asili ya kigeni, na ambao hawana vitambulisho wala stakabadhi zozote za uhamiaji. Haya yanaripotiwa huku kundi la Al Shaabab likitangaza kuhusika na mashambulizi hayo, japo idara ya polisi nchini imepuuza kauli hizo
Posted on July 5, 2012 na Alfrique Otieno
