Hatuhitaji sheria za trafiki
Posted on 23 May 2012 na Bernard Oginga
Tangu kulipochipuza taarifa kuwa sheria ya trafiki nchini Kenya itafanyiwa mabadiliko, kumekuwa na mazungumzo yanayoashiria matumaini kuwa mabadiliko hayo yatachangia pakubwa katika kupunguza visa vya ajali za barabarani ambavyo kwa sasa takwimu zinaonyesha huwaangamiza takriban Wakenya 3, 800 kila mwaka.
Binafsi nina maoni tofauti, kwamba sheria pekee hazitoshi kupunguza ajali wala vifo vinavyotokea barabarani. Ingawa marekebisho yanayonuiwa kufanyiwa sheria hiyo ni ya kuiboresha ili kuimarisha ufaafu wake katikika enzi hii ambapo idadi ya magari imeongezeka, barabara kuwa nzuri na uhayawani wa madereva pia kuzidi, durusu katika sheria inayotaka kurekebishwa inaonyesha kwamba kuna mengi chungu tele ambayo kama yangefuatiliwa kwa umakini unaofaa, usafiri barabarani na hasa katika magari ya umma ungekuwa wa kufurahisha acha ajali.
Unafahamu kwamba ni hatia kwa utingo (kondakta) kumsumbua dereva kwa mazungumzo au jambo jingine lolote anapokuwa usukani? Hii ni kulingana na kifungu cha 65(a) cha sheria ya trafiki inayotumika sasa.
Huenda katika pilka pilka zako za usafiri wa umma umewahi kukumbana na abiria ambao hung’ang’ana na wenzao kwenye mlango wa gari (kama si wewe mwenyewe) wanaposhuka au kupanda. Tabia kama hiyo imeharamishwa pamoja na kuingia garini kupitia sehemu nyingine yoyote isipokuwa mlangoni. Kifungu cha 66(c) cha sheria ya trafiki toleo la 2009 imepiga marufuku tabia kama hizo na nyinginezo ikiwemo kuchafua gari la usafiri wa umma.
Ukiukaji wa makatazo haya na mengine yaliyo katika sehemu ya sita (VI) inayosimamia mienendo ya madereva, utingo, na abiria katika uchukuzi wa umma unafaa kuadhibiwa kwa faini isiyopungua sh10,000 na isiyozidi sh15,000 au kufungo kisichozidi miezi sita gerezani.
Labda utadhani kwamba sheria iliyo sasa ni nzuri kwa kudumisha nidhamu na ushwari katika usafiri wa umma na kwamba imesahau kero kuu la ajali zinazosababisha mauti kila kukicha. Hebu tafakari hili; anayesababisha kifo kutumia gari anafaa kufungwa gerezani kipindi kisichozidi miaka kumi na kupokonywa kibali cha kuendesha kwa miaka 3 anapotoka gerezani (kifungu cha 45). Ikiwa hili linafuatwa kwa ukamilifu wake ni suala la kutiliwa shaka.
Ulevu ambao umetajwa kuwa kisababishi kikuu cha ajali barabarani pia unadhibitiwa na sheria ya sasa hivi kwamba ni hatia kumwuzia au kumpa dereva wa gari la umma kileo akiwa kazini. Licha ya kuwa adhabu ya ulevi au kumpa dereva kileo ni faini isiyozidi sh15,000 au kifungo cha miaka miwili gerezani au vyote viwili, matukio ya madereva kuzawadiwa kwa pombe wanapowapeleka abiria kwenye kituo fulani cha biashara ni mambo ya kila siku.
Ikiwa imekuwa kibarua cha kujaribu kuteka maji kwa gunia kutekeleza sheri hizi, je itawezekana vipi kuhakikisha kwamba kila dereva anayejipenyeza kandokando ya barabara na katika vituo vya kuuza mafuta ili kukwepa msongamano anakamatwa na kuadhibiwa kwa kutozwa faini ya sh30,000 kufungwa miezi mitatu au vyote?
Kibarua kingine kitakuwa kutekeleza adhabu ya faini ya laki tano au miaka kumi gerezania au vyote kwa watakaopatikana wakiendesha magari wakiwa walevi. Hili likifaulu, labda mauti yanayosababishwa na madereva walevi yatapungua.
Marekebisho hayo pia yanapania kukiondoa kikosi cha polisi wa trafiki na kuwapa kibali na uwezo polisi wowote kutekeleza jukumu la kuhakikisha sheria za barabarani zinafuatwa.
Kwa sababu ni bayana kuwa kanuni na sheria zipo, bila shaka tatizo lipo katika utekelezaji. Labda mawaziri watakaoteuliwa baada ya uchaguzi mkuu ujao kwa sababu hawatakuwa wanasiasa kama ilivyopendekezwa na katiba wataweza kutekeleza sheria kwa kina chake.
Tatizo si sheria, ni utekelezaji.
Jisomee sheria ya trafiki hapa...
http://www.kenyalaw.org/Downloads/GreyBook/11.%20The%20Traffic%20Act.pdf
Nyimbo Zilizochezwa Hivi Karibuni
| Mfupi | ||
| LORD EYEZ PA.mp3 | ||
| Bina na Ngai na Respect | ||
| Ya Nini Malumbano | ||
| Nyako Konya | ||
| News Intro | ||
| Let's Get down | ||
| Zanzibar | ||
| MAISHA ASUBUHI - SOUNDBED | ||
Video Za Kata Rumba
Showing: Overall


