Tupe ajenda zako, sio za wapinzani wako!

Posted on 18 May 2012 na Kizito Namulanda

Huku ikisalia miezi kadhaa kabla ya kutimia wakati ambapo Wakenya watapiga kura kumchagua Rais na viongozi wapya, tumeona hali ya mshikemshike hasa kwa wanasiasa wanaotaka kuwania urais ikianza kushika kasi. Sidhani nitakuwa nimekosea kusema kwamba tayari mbio za kutafuta kura za kuingia ikulu zimekwishaanza. Hili ni sawa, japo kuna tatizo.
Nimekuwa nikikereka sana kuwaona viongozi wanaojidai wanataka kuiongoza nchi hii wakijishughulisha zaidi na mambo yasiyofaa. Itakuwaje mtu anayetaka kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya awe kila mara anapopata jukwaa kuwazungumzia Wakenya iwe anajishughulisha tu viongozi wapinzani. Ikiwa si matusi, ni madharau ama majigambo! Mbona wasiitumie fursa kama hiyo kuwaeleza Wakenya kile watakachofanya iwapo watakabiliwa fursa uongozi. Je, mwelekeo wao kwa taifa hasa ni upi?
Naelewa vyema kwamba kumchachawisha na kumkosesha usingizi na hata kumlezama mpinzani wako kivyovyote vile siku zote huwa ni njia mojawapo ya kupata ushindi katika mashindano yoyote yale. Lakini swala hapa ni je, njia hii ndio mwafaka kwa wanasiasa wanaotaka uongozi nchini?
Sidhani jibu la swali hili ni ndio. Nionavyo mimi, wanasiasa wetu wameshindwa kubadilika. Wamesalia katika makovu ya siasa za kale wasijue kwamba hali imebadilika. Kwa tathmini yangu, wanachohitaji Wakenya sasa ni mtu atakayewashawishi kwamba atabadili mambo na wala sio ukalulu wa kushindana na kutukanana hadharani.
Nikirejelea mafunzo ya babu yangu nakumbuka hadithi ya wavulana wawili wanaoshindania msichana mrembo kijijini. Nilielimishwa kwamba ukishindania msichana ni sharti kila fursa uipatayo kumzungumzia umshawishi jinsi utakavyomfaa yeye na wala sio jinsi mpinzani wako asivyomfaa. Maanake ukimzungumzia sana kumhusu mpinzani wako, utampa shauku kubwa ya kutaka kujua zaidi kuhusu mvulana unaeshindana naye. Akitaka zaidi kujua ikiwa unayoyasema ni kweli ama la, itabidi azungumze naye.  Na ikiwa kila mara mtakapoachana msichana mrembo unayemtamani utakuwa umemjaza shauku ya kutaka kuzungumza ama kusikia zaidi kuhusu mpinzani wako, basi elewa kwamba kazi utakayokuwa ukiifanya ni sawa kuchota maji kutumia pakacha.
Ushauri wangu kwa viongozi wote wanaotafuta uongozi nchini Kenya ni huu, endapo utapata fursa yoyote kuwazungumzia Wakenya, jizungumzie wewe binafsi, wala usiwazungumzie wapinzani wako kwani ukifanya hivyo utakuwa ukiwafaidi wapinzani bila kujua.

Comments in chronological order (Total 0 comments)



1100 characters remaining

Nyimbo Zilizochezwa Hivi Karibuni

 
  Mfupi  
  LORD EYEZ PA.mp3  
  Bina na Ngai na Respect  
  Ya Nini Malumbano  
  Nyako Konya  
  News Intro  
  Let's Get down  
  Zanzibar  
  MAISHA ASUBUHI - SOUNDBED  

Video Za Kata Rumba

Skiza Kata Rumba Library2,726 Artists in total
Showing: Overall