Watu 'Wazuri' wanaimaliza Kenya
Posted on 3 May 2012 na Kizito Namulanda
Baada ya kujikuna na kutafakari kwa muda kutafuta suluhu ya shida za nchi yetu tukufu ya Kenya, hatimaye nafikiri nimepata jawabu. Jawabu la matatizo yanayoikumba Kenya. Na itakushangaza kwamba jawabu lenyewe si Katiba mpya ama viongozi wazuri kama wengi tunavyofikiria.
Tatizo la Kenya na ambalo litaendelea na hata hali kuwa mbaya zaidi ikiwa halitashughulikiwa ni kuwa watu wazuri; watu ambao ni werevu darasani; watu ambao ni maprofesa na madaktari; watu matajiri waliotunukiwa Baraka za kuwa na mali, wamekataa kuzaa watoto wengi.
Labda unashangaa nimeafikia vipi uamuzi huu. Siku moja baada ya kufanya kazi hadi mwendo wa saa tatu usiku nikielekea nyumbani, niliamua kupitia kwenye mkahawa mmoja katika mtaa wa kifahari wa Karen hapa jijini Nairobi ili kujipumbaza kidogo, ama kupigia mwili pole kama anavyopenda kusema mshamba Zebedayo.
Nilipoingia mkahawani nilipata meza yenye watu watatu, nami nikajiunga nao kuwa mtu wa nne kwa walikuwa watu tunaofahamiana nao. Kumbuka mitaa ya kifahari kupata watu zaidi ya kumi mkahawani wakati kama huo si rahisi.
Hata kabla ya kutulia, nilibaini kulikuwepo na mjadala mkubwa kati ya watu hao watatu. Kulikuwepo na jamaa mmoja ambaye alikuwa ameushikilia msimamo uliowashangaza wenzake.
Msimamo wake ni kwamba watu wazuri nchini; madaktari; maprofesa; watu wenye akili nyingi zenye maarifa; watu walio na mali na uwezo wa kuwalipia watoto karo hadi Vyuo Vikuu wanaendelea kuiharibu mbegu yao nzuri kwa kukosa kuzaa. Wameushikilia msimamo wa kuzaa tu watoto wawili basi ama wengine hata mmoja, badala ya kuzaa watoto sita wanane au hata kumi. Msimamo wake ni kwamba watu kama hawa wakiwazaa watoto watakuwa werevu sana na pia wataweza kuwasomesha hadi kufikia kiwango chochote watakacho. Kwa hivyo Kenya itakuwa bora zaidi, kwani itajazwa na watu wenye mbegu nzuri.
Badala yake wanaozaa watoto wengi ni watu wa mashambani ambao hata hawakufika vyuo vikuu ambao hawana mbegu ya uerevu ama mali ya kutosha. Na hata wakiwa na mbegu nzuri ya uerevu, watu wa mashambani na mitaa ya mabanda hawana uwezo wa kuwasomesha watoto hao hadi vyuo vikuu na hivyo wanaishia tu kusalia kwenye vijiji na talanta zao kupotelea kwenye pombe zisizo halali kama vile busaa na chang’aa.
Baada ya kutafakari kwa kina, nafikiri ni kweli kabisa, ikiwa watu wazuri wangeijaza Kenya kwa watoto wazuri, basi Kenya ingejaa watu wazuri, na shida zetu zote zingemalizika. Wanasema Waswahili kwamba mtoto wa nyoka ni nyoka.
Nyimbo Zilizochezwa Hivi Karibuni
| Mfupi | ||
| LORD EYEZ PA.mp3 | ||
| Bina na Ngai na Respect | ||
| Ya Nini Malumbano | ||
| Nyako Konya | ||
| News Intro | ||
| Let's Get down | ||
| Zanzibar | ||
| MAISHA ASUBUHI - SOUNDBED | ||
Video Za Kata Rumba
Showing: Overall


