Kesi
Ni ardhi tofauti; asema Moi
Rais Mustaafu Daniel Arap Moi amezungumzia uamuzi wa mahakama ya rufaa mjini Nakuru kuhusiana na sehemu ya ardhi ya taasisi maarufu ya Kabarak. Rais mustaafu amesema kwamba ardhi iliyohusishwa kwenye kesi hiyo ni tofauti na ardhi iliyojengwa Chuo kikuu cha Kabarak, Shule ya Sekondari ya Kabarak na makao ya jamii ya Kabarak. Kwenye taarifa rasmi iliyotumwa na msemaji wake Lee Njiru Mzee Moi ameihakikishia jamii ya Kabarak, wazazi wenye watoto Chuoni na shuleni kuwa shughuli kwenye taasisi hiyo hazitatatizwa. Rais Mustaafu amesema taasisi ya Kabarak inajumuisha Chuo, Shule ya Sekondari, ya Msingi na shule ya chekechea. Majaji wa mahakama ya rufaa Martha Koome na Hannah Okwengu wakiketi mjini Nakuru waliagiza kwamba rais Mustaafu arejeshe ardhi yenye ukubwa wa ekari 100 katika eneo la Kabarak kwa mlowezi Malcom Bell katika muda wa miezi sita kutoka sasa.
Posted on August 10, 2012 na Wellingtone Nyongesa
