Bunge
Ukumbi mpya wa bunge wafunguliwa
Rais Mwai Kibaki amefungua rasmi ukumbi mpya wa bunge uliokarabatiwa kwa gharama ya shilingi milioni 950. Ukumbi huo ulio na teknolojia ya hivi punde zaidi una uwezo wa kukaa wabunge 350 na studio ya kupeperusha matangazo ya radio na runinga moja kwa moja. Akizungumza katika ufunguzi huo rais hata hivyo amewashauri wabunge kujitolea kuwatumikia wananchi akisema ukumbi mpya na wa kisasa zaidi hautawafaa iwapo utendakazi hautakuwepo. Kibaki vile vile ametoa wito kwa wabunge wa sasa kuwania nyadhifa za ubunge akisema licha ya ugatuzi, bunge la taifa litakuwa muhimu na linahitaji watu wenye uzoefu kushirikiana na mawaziri ambao hawatakuwa wabunge. Spika wa Bunge Kenneth Marende amesema uamuzi wa kulipa idara ya gereza tenda ya kutengeneza viti ulilisaidia bunge kuokoa nusu ya fedha zilizokuwa zimeitishwa na makampuni ya ng’ambo. Rais kibaki amelikabidhi bunge katiba aliyotia saini wakati wa kuidhinishwa rasmi kwa katiba pamoja na kalamu aliyotumia ili kuhifadhiwa kama dafina ya taifa
Posted on August 7, 2012 na Bernard Oginga
