Mauwaji
Balozi auawa Nairobi
Kaimu balozi wa Venezuela nchini Kenya Olga Fonseca ameuawa na watu wasiojulikana. Kitengo cha polisi wanaoshughulikia usalama wa maafisa wa kibalozi nchini Kenya kimeupata mwili wa balozi huyo mwenye umri wa miaka 57 nyumbani kwake katika mtaa wa Runda. Balozi huyo amewasili nchini Julai 15 kuchukuwa mahala pa mtangulizi wake Gerardo Carrillo ambaye aliondoka Kenya baada ya wafanyakazi wa kike kwenye ubalozi wa Venezuela kumtuhumu kwa dhuluma za kimapenzi. Afisa mkuu wa polisi Nairobi Area Antony Kibuchi amesema kuwa ishara zote zinaonyesha kuwa balozi huyo alinyongwa nyumbani kwake alfajiri. Amesema kwamba polisi wanachunguza masuala mbali mbali kuhusiana na kifo hicho ikiwemo habari kuwa huenda wafanyakazi aliofuta kazi wamekuwa na kisasi naye. Balozi huyo aliwafuta kazi baadhi ya wafanyakazi waliodai mtangulizi wake alikuwa akiwadhulumu kimapenzi. Tayari wafanyakazi wawili wa ubalozi huo wametiwa nguvuni
Posted on July 27, 2012 na Wellingtone Nyongesa
