Siasa
MRC wakabiliwe, wanaharakati washinikiza
Serikali ya Kenya inazidi kupokea shinikizo la kutolitambua wala kufanya majadiliano na kundi la Mombasa Republican Council. Shinikizo la hivi karibuni limetolewa na kundi la vijana kwa jina Young Kenya Patriots ambalo limefanya maandamano kati kati mwa jiji la Nairobi kupinga uamuzi wa Mahakama kuu wa kuhalalisha kundi hilo. Msemaji wa kundi hlo la vijana Mark Moses Maina amesema MRC wanapaswa kushikizwa kukomesha kampeni zao zinazoongozwa na mwito wa PWANI SI KENYA. Wakiwa wamebeba mabango, mamia ya vijana hao wameandamana hadi Afisi ya Rais na Waziri Mkuu ambapo wametoa waraka kwa afisi hizo huku wakiwataka vinara hao kutokubali mkoa wa Pwani kijitenga na mikoa mingine ya Kenya. Wameelezea uungaji mkono wao kwa hatua ya Afisi ya mwanasheria mkuu wa serikali kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo. Maandamano haya yanajiri siku moja tu baada tofauti kuonekana kuzuka kati ya waziri mkuu Raila Odinga na kaimu waziri wa usalama Yusuf Haji kuhusu uwezekano wa serikali kushauriana na kundi hilo.
Posted on July 27, 2012 na Mate Tongola
