Mahakama
IEBC Inaweza Kuendelea na Mipango ya Uchaguzi
Tume ya uchaguzi na uratibu wa mipaka IEBC imeshinda katika kesi zilizowasilishwa mahakamani kupinga mipaka ya maeneo bunge mapya 80 na wodi 1,450. Katika uamuzi wa jopo la majaji watano liliyoteuliwa kusikiliza kesi hizo maeneo bunge yote mapya hayajaathirika.
Katika uamuzi huo uliochukua zaidi ya saa saba kusoma, mipaka ya maeneo bunge mapya iliyopendekezwa na IEBC itasalia hivyo kuongeza idadi ya maeneo bunge hadi 290. Hata hivyo baadhi ya mipaka za wodi zimejumuishwa huku mingine ikiondolewa.
Uamuzi huu umefungua ukurasa mpya katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu huku ikitarajiwa IEBC itaanza mikakati ya kuanda uchaguzi katika maeneo bunge hayo mapya. Hata hivyo uamuzi huo haujawafurahisha wengi huku baadhi ya mawakili wakitarajiwa kuwasilisha kesi katika mahakama ya rufaa kupinga uamuzi huo. Lakini kulingana na wataalamu wa sheria haiwezekani kukata rufaa ikizingatiwa muda wa siku 90 inayotolewa na sheria ya uchaguzi kwa kesi kuwasilishwa mahakamani unakamilika Jumanne.
Posted on July 9, 2012 na Alfrique Otieno
