PODCASTS

Habari

  • ICC

    UN haina usemi katika kesi za ICC, LSK

    Huku habari zikichipuka za kuonyesha kwamba huenda serikali ya jubilee imeanza kutoa misimamo tofauti kuhusu suala la ICC, Mawakili wa humu nchini sasa wanasema kwamba Umoja wa Mataifa hauna uwezo wa kuingilia utaratibu wa kesi katika Mahakama hiyo. Mwenyekiti wa LSK Eric Mutua amesema kwamba almradi kesi zimeanzwa kusikizwa katika mahakama hiyo umoja wa mataifa una uwezo wa kuomba tu kuahirishwa kesi. Mwenyekiti huyo ameyasema hayo siku moja tu baada ya wakili wa naibu Rais William Ruto, Karim Khan, kunukuliwa akisema kwamba waraka uliowasilishwa katika umoja wa mataifa haukuwakilisha msimamo wa serikali. Khan amesema mteja wake anaheshimu majaji wa ICC na hawezi kuunga mkono hatua kama hiyo. Aidha LSK inasema hatua hiyo inaashiria kuwa waraka uliotumwa umoja wa mataifa unakosa uzito.

    0 Responses

    Posted on May 10, 2013 na Apopo Mujema

  • Mahojiano

    Charity Ngilu Kuhojiwa

    Kigogo wa muungano wa Jubilee Charity Ngilu ni miongoni mwa mawaziri watano wateule walioratibiwa kuhojiwa ijumaa. Ngilu aliyeteuliwa kuongoza wizara ya ardhi na Nyumba anatarajiwa kukabiliwa na masuali magumu ikiwemo sakata za ufujaji wa mamilioni ya fedha iliyokumba wizara ya maji wakati akiwa waziri. Mahojiano hayo yanayoongozwa na spika wa bunge la taifa Justin Muturi yaling'oa nanga alhamisi ambapo mawaziri wateule watano walihojiwa akiwemo Henry Rotich waziri mteule wa fedha. Henry alitakiwa kuelezea jinsi atasuluhisha suala ya kupunguzwa kwa kiwango cha riba kinachotozwa na taasisi za fedha. Vile vile waziri mteule wa Ulinzi Raychelle Omamo alihojiwa na kujibu masuali ikiwemo jinsi atahakikisha uwazi kwenye ununuzi wa vifaa vya jeshi na suala la ufisadi katika usajili wa makurutu. Wengine waliohojiwa ni Ann Waiguru waziri mteule wa Ugatuzi na Prof Jacob Kaimenyi waziri mteule wa elimu.

    0 Responses

    Posted on May 10, 2013 na Mate Tongola

  • Usalama

    UN wataka usalama uimarishwe Bungoma

    Umoja wa mataifa umeitaka serikali ya Kenya kuingilia kati na kukomesha mashambulizi yakiwemo mauaji yanayoshuhudiwa katika kaunti za Busia na Bungoma. Katika taarifa, iliyotiwa sahini na mshirikishi wa masuala ya binadamu Modibo Toure, Umoja huo umeahidi kufuatilia kwa karibu ghasia hizo. Haya yanajiri wakati naibu rais William Ruto akizuru Bungoma na kuandaa mkutano na wakuu wa usalama katika kaunti hiyo na Busia kujadili visa vya utovu wa usalama. Kwenye mkutano huo ambao unahudhuriwa na machifu na wakuu wa polisi kwenye kaunti hizo, Ruto amewataka vongozi hao kuelezea hatua walizochukua kuhakikisha kuwa usalama unarejea. Hadi kufikia sasa zaidi ya watu kumi wameuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa katika mashambulizi hayo. Ni alhamisi wiki hii ambapo inspekta mkuu wa polisi alitangaza zawadi ya shilingi laki moja kwa yeyote atakayetoa taarifa kumhusu mfadhili wa mashambulizi hayo.

    0 Responses

    Posted on May 10, 2013 na Mate Tongola

  • Uchujaji

    Mawaziri wateule wahojiwa

    Shughuli ya kuwachuja mawaziri wateule 16 inaendelea katika jumba la mikutano la KICC, Nairobi. Tayari Mawaziri wateule Anne Waiguru, Raychelle Omamo wamehojiwa. Aidha licha ya kutangaza kujiondoa kwa wabunge wa muungano wa CORD kwenye kamati mbalimbali za bunge, wamejumuika na wenzao wa jubilee kwenye mahojiano hayo. Baada ya kuhojiwa Waziri mteule wa Ugatuzi na mipango Anne Waiguru, mwenzake wa Ulinzi Raychelle Omamo na Amina Mohammed wa mashauri ya nchi za kigeni kamati hiyo imemhoji pia waziri mteule wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Jacob Kaimenyi

    0 Responses

    Posted on May 9, 2013 na Mate Tongola

  • Mazishi ya Mutula

    Uhuru aongoza wakuu kumsifu Mutula

    Rais Uhuru Kenyatta amewaongoza viongozi wa kisiasa, mawakili na wakenya mashuhuri kumlimbikizia sifa kedekede hayati Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo. Imekuwa kwenye hafla ya mazishi yake Mei 9 katika shule ya Kima Mbooni kaunti ya Makueni. Uhuru ameiahidi familia ya Mutula ufadhili wa serikali kwa namna yeyote ile kwa heshima ya hayati seneta huyo. Kiongozi wa muungano wa Cord aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga amesema ili kuonyesha fadhila kwa hayati Mutula serikali inapaswa kujenga barabara ya lami hadi eneo hilo, amesema limekuwa ombi la hayati ambaye ametoa huduma ya kufaa kwa serikali ya Kenya. Rais Mustaafu Mwai Kibaki ameisifu familia ya hayati akiitaja kuwa iliyoelimika vyema na yenye uwezo wa kushiriki vyema kwenye masuala ya maendeleo ya taifa. Rais Mustaafu Moi alituma risala na kumtaja kuwa rafiki mkuu. Mutula alikuwa wakili wa rais Moi kwa zaidi ya miaka 20.

    0 Responses

    Posted on May 9, 2013 na Wellingtone Nyongesa

  • Ugatuzi

    Serikali za kaunti zatengewa Kshs 210B

    Serikali za kaunti zimetengewa kima cha shilingi bilioni 210. Hii ni kufuatia malalamishi ya wabunge na magavana kwamba shilingi bilioni 154 zilizokuwa zimetengewa serikali hizo hazitoshi. Akitangaza haya, naibu rais William Ruto amesema kuwa hazina kuu ya serikali imekubali kutoa fedha hizo baada ya kujadiliana na tume ya ugavi wa mapato ya serikali CRA. Awali, tume hiyo ilikuwa imependekeza kima cha shilingi bilioni 231 kutengewa serikali za kaunti dhidi ya shilingi bilioni 154 zilizokuwa zikipendekezwa na hazina kuu ya serikali. Kwenye ugavi wa fedha hizo, shilingi bilioni 190 zitagawanywa kwa kaunti zote 47 kuambatana na mfumo uliotolewa na tume ya CRA.

    0 Responses

    Posted on May 9, 2013 na Mate Tongola

  • Michezoni

    Sir Alex Ferguson kustaafu

    Mkufunzi wa klabu ya Manchester United Sir Alex Ferguson atastaafu mwishoni mwa msimu kama kocha wa klabu hiyo baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka 26, Ferguson mwenye umri wa miaka 71 chini ya uongozi wake ameshinda mataji 38 likiwemo lile la ligi kuu ya premier msimu huu baada ya kuchukua hatamu ya ukufunzi kutoka kwa aliyekuwa kocha wa klabu hiyo Ron Atkinson Novemba tarehe 6 mwaka wa 1986. Katika taarifa yake Ferguson amesema kwamba uamuzi wake wa kustaafu ni jambo moja ambalo amewazia kwa mda mrefu hivyo hatua yake ya kustaafu si jambo geni kwake. Ferguson aidha amesema kwamba lilikuwa ombi lake kustaafu ikiwa bado misingi ya klabu ingali dhabithi na anaamini kwamba hilo amefanikisha. Baada ya kustaafu kwake Ferguson anatarajiwa kuteuliwa kama mkurugenzi mkuu wa Manchester United pamoja kuijaza nafasi ya Balozi wa klabu hiyo,

    0 Responses

    Posted on May 8, 2013 na Apopo Mujema

  • Usalama

    CORD yadai kuwepo kwa njama

    Muungano wa CORD sasa unadai kuwa kuna njama ya kuwahusisha viongozi wa muungano huo na visa vya utovu wa usalama vinavyoshuhudiwa katika kaunti za Bungoma na Busia. Hii ni kufuatia kuhojiwa nduguye seneta wa bungoma Moses Wetangula, Fred Wetangula mapema jumatatu, saa chache tu baada ya mauaji kuripotiwa eneo hilo. Polisi aidha wamedokeza kuwa aliyeuwa mbunge wa Bumula Wakoli Bifowli aliandikisha taarifa kuhusu mauaji hayo ya watu 8. Aidha, imebainika kuwa Fred Wetangula ametakiwa kuripoti katika kituo cha polisi cha Bungoma kila siku. Haya yanajiri wakati maafisa zaidi wa polisi wametumwa katika kaunti hizo mbili kuimarisha usalama, siku moja tu baada ya watu 6 kujeruhiwa vibaya na watu wanaoshukiwa kuwa majambazi katika mtaa wa Ten Star karibu na Mji wa Bungoma. Mapema wiki iliyopita, watu 8 waliuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa.

    0 Responses

    Posted on May 8, 2013 na Mate Tongola

  • Kesi ICC

    Mashtaka Mapya Dhidi ya Uhuru

    Mkuu wa Mashtaka wa Mahakama ya Mataifa Kuhusu Uhalifu, ICC Fatou Bensouda ameyafanyia marekebisho mashtaka yanayomkabili Rais Uhuru Kenyatta kwa kuongeza ushahidi mpya. Hatua hii inamaanisha kuwa mashtaka dhidi ya Uhuru sasa yanahusisha visa vya watu kupigwa risasi katika miji ya Naivasha na Nakuru mwaka 2008, wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi. Ushahidi huo mpya unasema kuwa kundi la Munguki pamoja na vijana wa PNU walisafirishwa hadi maeneo ya Kaptembwa, Kwarhoda, Mwariki, Free Area na Kiti eneo la Nakuru kuwashambulia kwa silaha mbalimbali zikiwamo bunduki, panga, visu, mabomu ya petroli na hata vipande vya chupa, watu waliodhaniwa kuwa wafuasi wa chama pinzani. Inadaiwa kuwa baadhi ya waathiriwa walikatwa vichwa na sehemu nyingine za mili ili kuondoa alama zilizosababishwa na risasi. Mwezi Machi mwaka huu, mahakama ya ICC yalimpa kibali Bensouda kufanyia marekebisho mashtaka yanayomkabili Uhuru, huku aliyekuwa mshtakiwa mwenza Balozi Fransis Muthaura akiondolewa hatiani.

    0 Responses

    Posted on May 8, 2013 na Geoffrey Mung'ou