Wanasiasa na polisi walaumiwa kwa ukiukaji wa sheria za trafiki

Na Carren Omae
Kufuatia kuongezeka kwa ajali za barabarani hasa jijini Nairobi kutokana na kile kinachotajwa kuwa utepetevu wa madereva, Mamlaka ya Usalama Barabarani NTSA, imesema magari yote ya uchukuzi wa umma yanafaa kufuata kanuni za vyama vyao vya ushirika. Kwenye kikao na wanahabari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Francis Meja, amesema vyama hivyo vina mamlaka ya kuwaadhibu madereva wanaokiuka kanununi zao, vilevile sheria za trafiki.
Meja amefichua kwamba usimamizi wa Chama cha Ushirika cha Ongataline, ulikiri kutokuwa na uwezo wa kuyathibiti baadhi ya magari hali iliyosababisha kufutiliwa mbali kwa leseni yake.
Mamlaka hiyo imesisitiza kwamba itaendelea kufutilia mbali leseni ya vyama vya ushirika ambavyo vimeshindwa kuyadhibiti magari yao.
Wakati uo huo, Chama cha Kitaifa wa Usalama Barabarani, National Road Safety Association, kimewalaumu baadhi ya wamiliki wa magari hayo kwa kulemaza juhudi za idara zilizopewa majukumu kuyadhibiti. Chama hicho kimedai kuwa mengi ya magari hayo yanamilikiwa na maafisa wa polisi na wanasiasa. David Njoroge ni Mwenyekiti wa chama hicho.