Usalama waimarishwa kwenye viwanja vya ndege nchini

Wanaohudumu kwenye Kaunti ya Lamu wamewaua kwa kuwapiga risasi washukiwa wanne wa kundi gaidi la Al Shabaab waliojaribu kulivamia eneo la Milimani karibu na Baure.
Kwenye taarifa ya Wizara ya Ulinzi, wanamgambo hao awali walifanya jaribio la kuivamia kambi ya wanajeshi eneo la Mangai. Roketi, maguruneti mawili na bunduki nne aina ya AK47 ni baadhi ya silaha zilizopatikana kutoka kwao.
Afisa mmoja wa jeshi hata hivyo alijeruhiwa kwenye makabiliano hayo. Msemaji wa Jeshi, Kanali Cyrus Obonyo amesema vita dhidi ya Al Shabaab vitaendelea kwa lengo la kuimarisha usalama nchini.
Hayo yakijiri, usalama umeimarishwa katika viwanja vya ndege humu nchini kufuatia kisa cha kuuliwa kwa watu arobaini na mmoja katika Uwanja wa Mataifa wa Ataturk, Uturuki usiku wa kuamkia leo. Idadi ya waliojeruhiwa imefika mia mbili thelathini na tisa. Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinet amesema kisa hicho kinaashiria kujitolea kwa magaidi kutatiza amani kote ulimwenguni.
Kwenye kisa tofauti, nchini polisi wamemuua kwa kumpiga risasi mshukiwa mmoja wa Ugaidi eneo la Malindi huku wawili wakitiwa mbaroni.
Washukiwa hao wamekamatwa baada ya awali kukwepa mtego wa polisi. Bunduki mbili zimepatikana kutoka kwao.

Na, Beatrice Maganga,

Related Topics