Mkenya awasilisha sababu za kutaka kubanduka kwa makamishna wa IEBC

Huku kamati ya pamoja inayowajumuisha wabunge na maseneta wa Jubilee na CORD ikitarajiwa kuanza mazungumzo kuhusu hatima ya makamishna wa Tume ya Uchaguzi IEBC, kamati ya Haki na Sheria Bungeni imeanza vikao rasmi vya kusikiliza ombi lililowasilishwa na mkazi wa Bungoma, Barasa Kundu Nyukuri kuwataka makamishna wa tume hiyo kuondoka ofisini. Vikao hivyo vinaanza baada ya kamati hiyo pamoja na ile ya Bunge ya Utekelezaji Katiba, CIOC kupokea ombi hilo rasmi leo hii.
Kwenye vikao vya leo, Nyukuri ameelezea sababu za kuwasilisha ombi hilo. Akijibu maswali ya wabunge, mlalamishi huyo amesema ni kupitia bunge tu ndipo utaratibu wa kuwaondoa makamishna hao utatekelezwa, huku akielezea haja ya shughuli hiyo kuharakishwa ili kutoa nafasi kwa makamishna wengine kuteuliwa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Ameiambia kamati hiyo kwamba IEBC haiwezi kusimamia uchaguzi mkuu ujao, akidai kwamba imeshindwa kuwasajili wapiga-kura, mbali na kutilia shaka uhuru wa tume hiyo.

Na, Caren Omae

Related Topics

IEBC